Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, ameipongeza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kwa namna inavyotekeleza majukumu yake kwa weledi na mchango wake katika kukuza maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini.
Pongezi hizo zilitolewa na Waziri Simbachawene alipotembelea banda la TAA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma, ambapo pia alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo kwa mwaka 2025.
Katika ziara hiyo, Waziri alipata maelezo kuhusu majukumu makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, ikiwa ni pamoja na kusimamia, kuendeleza na kuendesha viwanja vya ndege 61 vya serikali, vikiwemo viwanja viwili vya kimataifa vya Julius Nyerere (JNIA) na Kilimanjaro (KIA).
Aidha, Waziri Simbachawene alifahamishwa kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika viwanja vya ndege vya Msalato, Tabora, Shinyanga, Musoma, Kigoma, Sumbawanga, Moshi na Lake Manyara. Kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Msalato, Bw. Jeff Shentiwa alieleza kuwa miradi hiyo imelenga kuboresha huduma na miundombinu ili kuongeza ufanisi wa usafiri wa anga, na tayari baadhi ya miradi kama ile ya viwanja vya Iringa, Mtwara, Dodoma, Mpanda na Kahama imekamilika.
Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka huu yamebeba kaulimbiu isemayo “Utoaji wa Huduma kwa Wananchi: Dhamira ya Mabadiliko ya Kiutawala Barani Afrika,” ambapo taasisi mbalimbali za serikali, zikiwemo zilizopo chini ya Wizara ya Uchukuzi kama TAA, zinatumia jukwaa hilo kuonesha mafanikio yao na kuimarisha uhusiano na wananchi wanaowahudumia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza alipotembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Kiwanja Cha Ndege cha Kimataifa Msalato Bw. Jeff Shantiwa alipotembelea banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisaini kitabu katika banda la Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...