Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene, amepongeza Shirika la Mawakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa namna linavyotekeleza kwa ufanisi majukumu yake katika kusimamia sekta ya usafiri wa majini nchini.

Mhe. Simbachawene alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la TASAC katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma. Waziri huyo alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho hayo ambayo yanalenga kuonesha namna taasisi za umma zinavyotekeleza majukumu yao kwa uwazi, uwajibikaji na ufanisi.

Waziri Simbachawene alisisitiza umuhimu wa Shirika kama TASAC kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uwazi na ubunifu ili kuongeza mchango wa sekta ya usafiri wa majini katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira.

Akipata maelezo ya kina Waziri Simbachawene kutoka kwa Afisa Mkaguzi na Msajili Mkuu wa Vyombo vya Usafiri Majini kutoka TASAC, Bw. Said Mkwawa, alielezwa kuhusu majukumu ya msingi ya shirika hilo ambayo ni pamoja na kusimamia na kuratibu shughuli zote za uwakala wa meli nchini, kusajili na kukagua vyombo vya usafiri majini, kusimamia usalama na ulinzi katika usafiri wa majini, kutoa mafunzo na usajili wa mabaharia na kuwezesha utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kuhusu usafiri wa majini.

Bw. Mkwawa alieleza kuwa TASAC imeendelea kuboresha mifumo yake ya usimamizi na huduma kwa wananchi ili kuhakikisha usafiri wa majini unakuwa salama, unaotegemewa na unaochangia kikamilifu katika uchumi wa taifa, hususan maeneo ya kanda ya pwani na maziwa makuu.

Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yanafanyika kwa kaulimbiu isemayo “Utoaji wa Huduma kwa Umma kwa Msingi wa Maadili, Uwazi na Uwajibikaji kwa Maendeleo Endelevu,” ambapo taasisi kama TASAC zinatumia jukwaa hilo kuonesha mafanikio yao, kuelimisha wananchi, na kujenga uhusiano wa karibu kati ya serikali na wananchi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Mkaguzi na Msajili Mkuu wa Vyombo vya Usafiri Majini kutoka TASAC, Bw. Said Mkwawa kuhusu kazi mbalimbali za Shirika hilo alipotembelea Banda la Shirika la Mawakala wa Meli Tanzania (TASAC) wakati wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. Wa kwanza kushoto ni Afisa Uhusiano Mwandamizi TASAC Amina Miruko.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akipokea zawadi kutoka kwa Afisa Mkaguzi na Msajili Mkuu wa Vyombo vya Usafiri Majini kutoka TASAC, Bw. Said Mkwawa kwa niaba ya Shirika la Mawakala wa Meli Tanzania (TASAC) wakati wakati wa ufunguzi wa maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2025 yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...