Watoto wachanga nchini Tanzania wanatarajiwa kunufaika na maisha salama na yasiyo na maumivu kutokana na ubunifu mpya wa kiteknolojia wa mwanafunzi wa uhandisi tiba kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Abubakar Mathias, ambaye amebuni kifaa cha kisasa cha kupima kiwango cha manjano (bilirubin) bila kutumia damu.

Ubunifu huo, unaofahamika kama BiliMeasure, unaondoa hitaji la uchukuaji wa sampuli ya damu mchakato unaosababisha maumivu kwa watoto na wasiwasi kwa wazazi na badala yake hutumia sensa maalum kupima kiwango cha bilirubin kwa wakati halisi, moja kwa moja kutoka kwenye ngozi ya mtoto.

 “Kinavaa kifuani au kichwani wakati wa tiba ya mwanga (phototherapy), na hupima kiwango cha manjano mara moja bila kuchukua damu. Kinatoa majibu papo kwa hapo kwa daktari au mtoa huduma,” amesema Mathias.

Manjano kwa watoto wachanga ni hali ya kiafya inayotokana na kuongezeka kwa kemikali ya bilirubin mwilini. Ikiwa haitagundulika na kutibiwa mapema, inaweza kuathiri ubongo wa mtoto na kusababisha ulemavu wa kudumu au kifo. Kwa sasa, upimaji wa bilirubin unategemea sampuli ya damu ambayo huweza kuchukua hadi saa 24 kupata majibu na huhitaji vifaa vya gharama kubwa ambavyo havipatikani kwa urahisi katika vituo vya afya vya ngazi ya chini.

Mathias anaeleza kuwa kifaa cha BiliMeasure kimelenga kuleta mapinduzi katika huduma ya afya kwa watoto wachanga nchini, kwa kusaidia kupunguza ucheleweshaji wa matibabu, kuimarisha usalama wa watoto na kuongeza ufanisi wa utambuzi wa hali ya manjano.

“Kifaa hiki kitawezesha ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya mtoto wakati wa tiba bila kuchukua damu mara kwa mara, jambo ambalo pia hupunguza mzigo kwa wahudumu wa afya,” ameongeza.

Mradi huo wa bunifu umepongezwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya waliotembelea banda la MUHAS katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam, wakisema kuwa ni suluhisho la muda mrefu na rafiki kwa mazingira ya afya ya watoto wachanga, hasa katika maeneo yenye rasilimali chache.

Ubunifu wa BiliMeasure unaweka Tanzania katika nafasi nzuri ya kuongoza kwa suluhisho za kiafya bunifu barani Afrika, na unaonesha nguvu ya vijana wa kitanzania katika kutatua changamoto za kiafya kwa kutumia teknolojia rahisi na yenye ufanisi mkubwa.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...