WATOTO wengi wanaozaliwa na tatizo la mgongo wazi (spina bifida) hukumbwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kupooza kuanzia kiunoni, hali inayowanyima uwezo wa kusimama au kutembea. Mbali na athari hizo za kiafya, watoto hao hukabiliwa na changamoto za kijamii na kifamilia, ikiwemo utegemezi wa vifaa saidizi ambavyo si rafiki kwa ukuaji wao wa mwili na maendeleo ya kiafya.

Vifaa hivyo vya kawaida mara nyingi havibadiliki kadri mtoto anavyokua, vinaweza kusababisha vidonda vya muda mrefu kutokana na msuguano na havitoi taarifa yoyote ya maendeleo ya kimatibabu. Pia mzazi au mlezi hulazimika kubadilisha mara kwa mara vifaa hivyo, jambo linaloongeza mzigo wa kifedha.

Sasa, matumaini mapya yameibuka kupitia ubunifu wa Mhandisi Tiba Mercy Elisante Karekwa kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambaye amebuni kifaa cha kisasa cha roboti kiitwacho Robospine, chenye uwezo wa kubadili maisha ya watoto wenye mgongo wazi.

Robospine ni kifaa cha roboti kinachosaidia mtoto kusimama na kufanya mazoezi ya kutembea kwa muundo maalum unaojirudia (pattern), ambao huchochea ukuaji wa misuli na kuimarisha mifupa. Tofauti na vifaa vya kawaida, Robospine hujirekebisha kadri mtoto anavyokua, hivyo kinaweza kutumika kwa muda mrefu bila kuhitaji kubadilishwa mara kwa mara.

"Robospine kinamsaidia mtoto kuanzia hatua ya mwanzo kabisa kama kusimama na baadaye kufanya mazoezi ya kutembea kwa muundo unaojirudia, ambao husaidia kuimarisha misuli na mifupa," amesema Mercy.

Amesema kifaa hicho pia kimeunganishwa na vichunguzi vya misuli na shinikizo vinavyokusanya taarifa na kuziwasilisha moja kwa moja kwa walezi kupitia simu janja, hivyo kuwezesha ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo ya mtoto nyumbani au kliniki.

Mercy anasema lengo ni kuhakikisha ndani ya kipindi cha miaka miwili hadi mitatu, mtoto anaweza kuimarika hatua kwa hatua hadi kufikia kutembea mwenyewe bila msaada.

"Tunalenga kuona watoto wakijitegemea baada ya mazoezi ya kutosha. Katika hatua zijazo, tutaliunganisha kifaa na mfumo wa umeme utakaorekodi umbali wa kutembea na hatua alizopiga, hivyo kusaidia kufuatilia maendeleo ya afya na tiba kwa usahihi zaidi," ameongeza.

Robospine si tu linapunguza gharama kwa wazazi, bali linachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi wa huduma za afya kwa watoto wenye ulemavu wa viungo, na kuwajengea msingi wa kujitegemea katika maisha yao ya baadaye.

Ubunifu huu wa kitanzania ni mfano hai wa namna taaluma ya uhandisi tiba inavyoweza kubadilisha maisha na kusaidia jamii zilizo katika uhitaji mkubwa wa suluhisho la kiafya la muda mrefu na endelevu.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...