Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limetekeleza operesheni ya mafanikio usiku wa tarehe 22 Julai 2025 kwa kukamata boti aina ya fibre, rangi nyeupe, iliyokuwa ikisafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi kutoka nchini Kenya kupitia Bahari ya Hindi.
Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Almachius Mchunguzi, amesema kuwa boti hiyo ilikamatwa na Kikosi cha Polisi Wanamaji (Marine) katika eneo la Mawe Mawili, Kijiji cha Kwale, mpakani mwa Wilaya ya Mkinga na Jiji la Tanga, kufuatia taarifa za kiupelelezi na ufuatiliaji wa kina wa mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji haramu.
Kwa mujibu wa Kamanda Mchunguzi, watuhumiwa wawili waliokuwa kwenye boti walifanikiwa kutoroka baada ya kufika karibu na fukwe, lakini boti pamoja na shehena ya mirungi vilikamatwa.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeeleza kuwa litaendelea kuimarisha doria na operesheni maalum hususan katika maeneo ya baharini ambayo yamekuwa yakitumiwa na wahalifu kuvusha bidhaa haramu kutoka nchi jirani.
Aidha, Kamanda Mchunguzi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika jamii, hususan vinavyohusiana na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...