Farida Mangube, Morogoro.
Uchaguzi wa madiwani wa viti maalum kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Morogoro Mjini umeonesha mwelekeo mpya wa siasa za wanawake ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku sura mpya zikiibuka na kuonesha nguvu ya wajumbe, hoja na dhamira ya kweli ya uongozi.
Katika uchaguzi huo uliofanyika jana na kuhitimishwa alfajiri ya leo, wajumbe na wagombea walikesha wakishuhudia ushindani wa aina yake ulioambatana na nidhamu na mshikamano.
Matokeo yalitangazwa saa 12:15 asubuhi Juni 21, na msimamizi wa uchaguzi, Khalid H. King, ambaye ni Katibu wa UVCCM Morogoro Mjini.
Miongoni mwa wagombea waliopata kura nyingi ni Latifa Said Ganzel, mwandishi wa habari ambaye aliongoza kwa kuipata kura 934, akifuatiwa na Batuli Kifea (794), Grace Mkumbae (752), Salma Mbandu 698, Imakulata Mhagama 581 na Warda Bazia 562.
Wengine ni Rahma Maumba 560, Magreth Ndewe 556, Anna Kisimbo 535 na Amina Zihuye kura 532.
Miongoni mwa walioongoza kwenye kumi bora wamo madiwani sita waliotetea nafasi zao, huku sura maarufu za madiwani kama Hadija Kibati, ‘Mama Nyau’, Zamoyoni Abdallah, na Mwanaidi Ngulungu wakiondolewa kwenye kapu la kura kwa kura zao kutowafikisha 10 Bora.
“Wanawake wameonyesha kuwa wako tayari kubeba ajenda ya maendeleo na Ushindi wa kina, kwa Latifa si tu kura, ni sauti ya mabadiliko.”Alisema Anna Zuberi mjumbe kutoka kata ya Kingo.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, ushindi huu ni alama kwamba wanawake hawako tena nyuma kwenye uthubutu wa kushiriki uchaguzi bali mstari wa mbele pia katika kufanikisha Dira ya CCM 2030 na Ajenda ya Maendeleo ya Taifa kwa mtazamo wa jinsia.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...