Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI ya Tanzania imeendelea kuchukua hatua thabiti za kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika kwa ajili ya kuharakisha maendeleo ya viwanda na kuchochea ukuaji wa uchumi, kupitia mradi mkubwa wa usafirishaji wa umeme kutoka Chalinze hadi Kituo cha Kinyerezi III wenye urefu wa kilomita 135 na uwezo wa kusafirisha hadi megawati 1,000.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, amesema hayo leo Julai 10, 2025 jijini Dar es Salaam alipokuwa akikagua miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, I Extension na Kinyerezi II.

Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko ameeleza kuwa ujenzi wa njia hiyo mpya ya umeme ni sehemu ya mpango wa Serikali kuhakikisha nishati ya uhakika inafika katika maeneo ya viwanda, hususan katika mikoa ya pwani na magharibi, ambayo awali ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa kutosha.

 “Maeneo kama Mkuranga yana viwanda vingi yanayohitaji umeme wa kutosha. Hali hii inatufanya tuongeze uwezo wa vituo vya kuzalisha, mfano Kinyerezi III kutoka megawati 600 hadi 1,000 ili kukidhi mahitaji yanayoendelea kuongezeka,” amesema Dkt. Biteko.

Akizungumzia maendeleo ya upatikanaji wa umeme nchini, Dkt. Biteko amesema mafanikio yaliyopatikana hadi sasa yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mhe. Rais Samia amewekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya nishati. Kwa mwaka huu wa fedha, tumetenga Shilingi trilioni 2.3 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya umeme na kuimarisha miundombinu ya usambazaji,” amesema Dkt. Biteko.

Aidha, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa sekta ya nishati ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, na ndio msingi wa maendeleo ya viwanda, biashara, elimu, na huduma za afya.

Amepongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa maboresho makubwa ya huduma zake kwa wananchi, ikiwemo kuondoa gharama za simu kwa wateja wanaotaka msaada wa haraka na kuimarisha usikivu na ufuatiliaji wa changamoto za wateja.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi ya mwaka 2024, sekta ya nishati imekuwa kwa asilimia 14, ikishika nafasi ya pili nyuma ya sekta ya Sanaa, Utamaduni, Michezo na Habari ambayo imekua kwa asilimia 17.

Dkt. Biteko amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kushiriki katika ulinzi wa miundombinu ya umeme na kulipa gharama za matumizi kwa wakati, ili kuendeleza juhudi za Serikali katika kujenga taifa lenye nishati ya uhakika kwa wote.

Kwa Upande wa Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Endward Mpogolo amesema kuwa ziara hiyo ni ya muhimu sana kwa kuwa inatoa mwanga wa wazi kuhusu hali ya uzalishaji wa nishati nchini, hasa wakati huu ambapo mahitaji ya umeme yanaongezeka kufuatia ukuaji wa viwanda, hasa katika Wilaya ya Kigamboni.

"Ni hatua muhimu katika kuhakikisha huduma ya umeme inaimarishwa ili kuendana na kasi ya maendeleo," amesema Mpogolo.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya alitumia fursa hiyo kupeleka salamu za shukrani kwa Mheshimiwa Rais kwa kushughulikia kwa vitendo changamoto ya maji jijini Dar es Salaam.

"Tupelekee salamu kwa Mheshimiwa Rais kwa kuleta zaidi ya Shilingi bilioni 37 ambazo zimewezesha ujenzi wa tanki kubwa la maji lililopo Bangulo, Wilaya ya Ilala. Tenki hilo litakuwa sehemu muhimu ya kusaidia upatikanaji wa maji kwa wakazi wa jiji na pia litachangia katika upatikanaji wa umeme," ameongeza.

Vilevile, ameeleza shukrani kwa Serikali kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo katika wilaya mbalimbali za Dar es Salaam, jambo ambalo limechochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kuchangia ustawi wa nchi kwa ujumla.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo akizungumza wakati wa ziara ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko (wa tatu kulia) akikagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange akisalimiana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko wakati akiwasili katika miradi ya kuzalisha umeme leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam.
Mitambo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II.
 
Matuki mbalimbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...