Na Pamela Mollel, Arusha

Sekta ya kilimo imeelezwa kuwa mhimili mkubwa wa maendeleo ya viwanda nchini, ambapo asilimia 65 ya malighafi inayotumika viwandani hutokana na mazao ya kilimo

Aidha Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuipa sekta hiyo kipaumbele kikubwa kwa lengo la kuinua uchumi na maisha ya Watanzania.

Akizungumza jijini Arusha katika maonyesho ya 14 ya Siku ya Kilimo Biashara yaliyoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Selian, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mwinyi Ahmed Mwinyi amesema serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya kilimo kila mwaka kama ishara ya dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwaka 2021 bajeti ya Wizara ya Kilimo ilikuwa Shilingi Bilioni 294, mwaka 2022/2023 ikapanda hadi Bilioni 751, mwaka 2023/2024 Bilioni 970.8, mwaka 2024/2025 ni Trilioni 1.2 na mwaka 2025 bajeti imefika Trilioni 1.24.

Ameeleza kuwa maonyesho hayo ni jukwaa muhimu kwa wakulima na wadau wa kilimo kupata elimu, teknolojia mpya na mbinu bunifu zitakazosaidia kuongeza tija shambani.

"Kupitia maonyesho haya tumeweza kushuhudia bunifu mbalimbali za teknolojia kwa ajili ya kuongeza tija katika kilimo, ameongeza Mwinyi

Mkuu huyo wa wilaya pia amewapongeza wanawake kwa kuwa mstari wa mbele kwenye sekta ya kilimo, akisema wamekuwa mfano wa kuigwa kutokana na juhudi na ubunifu wao unaoleta mafanikio makubwa vijijini na mijini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TARI Dkt. Thomas Bwana amesema taasisi hiyo inalenga kuhakikisha tafiti zinazofanywa zinaendana na changamoto halisi za wakulima ili kuwawezesha kuzalisha kwa ufanisi.

Tunatamani kuona teknolojia zetu zinawafikia wakulima kwa wakati ili kutatua changamoto zao. Hii ndiyo sababu tunawashirikisha pia sekta binafsi zinazozalisha mbegu bora, amesema Dkt. Bwana.

Ameongeza kuwa maonyesho hayo yanatoa nafasi kwa wakulima kukutana na makampuni yanayozalisha pembejeo, taasisi za utafiti, wataalamu wa kilimo na wadau wengine muhimu katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Maonyesho haya ya Kilimo Biashara yamefanyika kwa mara ya 14 tangu yaanzishwe mwaka 2012, na yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuunganisha wakulima, makampuni ya pembejeo, taasisi za serikali, mashirika ya kimataifa na wadau mbalimbali wa maendeleo ya kilimo nchini.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...