Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia mchakato wake wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa ubunge kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kimelirudisha jina la Kada wake Amandus Jordan Tembo, maarufu kama Toronto, miongoni mwa majina matano yaliyopitishwa rasmi kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Songea Mjini.
Uamuzi huo umetangazwa jana, tarehe 29 Julai 2025, na Mwenezi wa CCM Taifa Amos Makala mara baada ya CCM kukamilisha uchambuzi wa awali wa wagombea waliokuwa wamechukua fomu na kufanyiwa usaili, Kupitishwa kwa jina la Toronto katika hatua hii ya awali ni hatua muhimu kwenye safari yake ya kisiasa, hasa ikizingatiwa kuwa hii ni mara yake ya kwanza kuwania nafasi ya Ubunge katika jimbo hilo.
Toronto, mwenye umri wa miaka 35, amekuwa akifahamika kwa jina hilo maarufu kutokana na historia yake ya elimu katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Canada, ni kijana ambaye amerejea nyumbani Songea akiwa na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi na kuchangia katika maendeleo ya kijamii na kisiasa ya jimbo hilo.
Katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni, Toronto ameendelea kujitokeza kwa kazi zake za kijamii na kisiasa, ikiwemo ujenzi wa ofisi za CCM kwa fedha zake binafsi katika Kata ya Subira (Tawi la Liwena) na Kata ya Bombambili, jambo lililoonyesha kwa vitendo uzalendo wake na imani yake kwa chama, Ujenzi huo umepongezwa sana na viongozi pamoja na wanachama wa CCM katika mkoa wa Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya jina lake kupitishwa katika hatua ya awali , Toronto alisema:
"Kupitishwa kwa jina langu ni heshima kubwa kwangu, familia yangu, na kwa vijana wote wa Tanzania wanaoamini kuwa mabadiliko yanawezekana kupitia siasa safi na ya vitendo. Ninaendelea kusimama kwa dhamira ileile niliyoiweka mbele ya wananchi wa Songea Mjini kuwatumikia kwa moyo wa uzalendo, uwazi na ufanisi."
Kupitia maono yake, Toronto ameweka mkazo kwa maendeleo ya kijamii, hususan katika sekta za elimu, afya, na ajira kwa vijana, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushiriki wa vijana katika siasa za kujenga, akiamini kuwa wakati wa viongozi wapya wenye maono, uadilifu, na uwezo wa kutenda umefika.
Kwa sasa, CCM inaendelea na hatua nyingine za mchujo kuelekea uteuzi wa jina moja litakalosimama kwa niaba ya chama katika uchaguzi wa Oktoba, hata hivyo, kupitishwa kwa Toronto katika hatua hii kunampa nafasi kubwa ya kusonga mbele, hasa kutokana na mvuto wake wa kisiasa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa wanachama wa chama hicho.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...