WANAWAKE nchini Tanzania wanatarajia kunufaika kwa kiasi kikubwa na ubunifu mpya uliobuniwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambao unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi—ugonjwa unaoendelea kuua maelfu ya wanawake kila mwaka nchini.
Katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam, maarufu kama Sabasaba, wanafunzi hao wamewasilisha kifaa maalum kinachomuwezesha mwanamke kujichukulia sampuli mwenyewe bila msaada wa daktari, pamoja na mfumo wa kidijitali unaochambua sampuli na kutoa majibu kwa haraka.
Godson Madeha, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika fani ya udaktari kutoka Chuoni hapo amesema kifaa hicho ni rahisi kutumia na humuepusha mwanamke na aibu au maumivu yanayoweza kujitokeza wakati wa uchunguzi wa kawaida.
“Mwanamke atachukua sampuli kwa kuingiza kifaa ukeni hadi kwenye alama maalum, kisha kukizungusha. Anaweza kufanya hivyo bila msaada wa daktari, na baadaye majibu atayapata kwa njia ya mtandao,” amesema Madeha
Madeha amesema wazo la ubunifu huo lilitokana na ongezeko kubwa la visa vya saratani ya mlango wa kizazi, sambamba na changamoto za uhaba wa vifaa na huduma za uchunguzi wa awali.
“Saratani hii inaua nguvu kazi ya taifa, na inaweza kutibika endapo itagunduliwa mapema. Tunalenga kuondoa vikwazo vya huduma hizi muhimu,” ameongeza.
Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Chuo hicho cha Muhas Lucy Kitambala, amesema wameunda pia mfumo wa kidijitali uitwao Akili Mnemba unaotumia teknolojia kuchambua sampuli na kubaini uwepo wa saratani, hatua iliyofikiwa, pamoja na seli zilizoathirika.
“Mfumo huu una ufanisi wa zaidi ya asilimia 95 na unaweza kumpatia daktari majibu ndani ya dakika mbili tu. Hii itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa na makosa ya kibinadamu,” amesema Lucy.
Ameongeza kuwa mfumo huo haumlazimu daktari bingwa ili kuutumia, bali unaweza kutumika katika ngazi zote za huduma kuanzia hospitali kubwa hadi vituo vya afya vya wilaya.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2022 zinaonyesha kuwa Tanzania iliripoti visa vipya 10,866 vya saratani ya mlango wa kizazi na vifo 6,832, huku ni asilimia 18 tu ya wanawake waliostahili kufanyiwa uchunguzi wakiwa wamepimwa angalau mara moja kwa mwaka.
Kwa ubunifu huu wa wanafunzi wa MUHAS, Tanzania inaelekea katika hatua mpya ya kuimarisha mapambano dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi, na hivyo kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...