Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Akizungumza leo jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa huduma mpya katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Mhagama amesema huduma hizo—zinazolenga watu mashuhuri, wagonjwa wa kimataifa na uchunguzi mkubwa wa kitaalamu—zinapaswa kuwa mfano kwa hospitali zote za Kanda, Maalum na Taifa.
“Hospitali ya hadhi hii inapaswa kuzipeleka huduma karibu zaidi kwa wananchi. Ninakubaliana kabisa na mpango wa hospitali kutafuta eneo mjini kwa ajili ya kliniki itakayohudumia wagonjwa wasiokuwa na uhitaji wa matibabu makubwa kama njia ya kupunguza foleni,” amesema Mhagama.
Katika hafla hiyo, Waziri Mhagama amehimiza ushirikiano baina ya taasisi za ndani ya nchi, akisema ni lazima taasisi zote za afya kushirikiana kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma na kuendeleza rasilimali watu waliopo.
Ameeleza kufurahishwa na hatua ya kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na hospitali za KCMC na JKCI.
“Ushirikiano huu unalenga kuimarisha uwezo wa taasisi zetu, kuongeza wigo wa huduma zinazopatikana hapa nchini, na kupunguza utegemezi wa huduma za nje,” amesema.
Waziri huyo pia amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia ya kisasa kama tiba mtandao (telemedicine) ili kurahisisha mawasiliano kati ya taasisi, kuwajengea uwezo wataalamu, na kuwapunguzia gharama wagonjwa wanaotafuta huduma za kibingwa.
Aidha, Mhagama ameeleza kufurahishwa na ushirikiano wa karibu kati ya Hospitali hiyo na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), hususan katika utekelezaji wa mradi wa Shilingi Bilioni 28 wa upandikizaji figo, unaofadhiliwa na Shirika la TOKUSHUKAI la Japan. Mradi huo unatarajiwa kuifanya Tanzania kuwa kituo kikubwa cha umahiri cha upandikizaji figo katika Afrika Mashariki, na ujenzi wake unaanza mwaka huu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema hospitali hiyo sasa inatoa huduma 17 za kibingwa na inapokea zaidi ya wagonjwa 1,200 kwa siku.
Prof. Makubi pia amebainisha kuwa hospitali hiyo imeanza kutoa huduma ya upandikizaji wa figo kutoka kwa mtu hai kwenda kwa mwingine bila kufungua tumbo, pamoja na upandikizaji wa uloto kwa wagonjwa wa selimundu (sickle cell) bila hitaji la kufanana damu.
“Tumeanza pia maandalizi ya ujenzi wa hosteli kwa ajili ya wanafunzi wa ngazi ya diploma kwa kutumia mapato ya ndani, na kwa kushirikiana na UDOM, tunatarajia kuandaa mkutano wa kitaifa kuhusu upandikizaji wa figo na uloto,” amesema Prof. Makubi.
Kwa ujumla, tukio hilo limeashiria hatua kubwa inayopigwa na sekta ya afya nchini kupitia usimamizi wa kisera, uwekezaji wa serikali, ushirikiano wa kimataifa na ubunifu wa ndani unaoelekezwa katika kuboresha maisha ya Watanzania.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...