Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Balozi Mobhare Matinyi, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Mhe. Maria Malmer Stenergard, katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Stockholm, leo tarehe 22 Agosti, 2025.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Balozi Matinyi aliwasilisha salamu kwa wananchi na Serikali ya Ufalme wa Sweden kutoka kwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye ni Mwanadiploamsia namba 1 nchini, na kusisitiza dhamira ya Tanzania kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia na ushirikiano wa kiuchumi na Sweden.

Vilevile, Balozi Matinyi alieleza juhudi za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha ustawi wa uchumi kupitia ushirikiano na Sweden, hususan katika sekta za nishati, elimu, afya, utafiti, mazingira, uzalishaji viwandani, na miradi ya miundombinu kama vile reli ya kisasa (SGR).

Katika mzungumzo hayo, Mhe. Balozi Matinyi alibainisha kuwa hadi sasa, jumla ya kampuni 101 kutoka Sweden zimewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali, zikiwa na thamani ya dola za Marekani milioni 313.04 na zikichangia ajira takribani 3,877 huku akisisitizia nia ya Tanzania kuimairisha biashara na uwekezaji baina yake na Sweden.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Mhe. Stenergard, alithibitisha dhamira ya Sweden kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Aidha, Waziri Stenergard alihimiza mchango wa Tanzania katika kudumisha amani na usalama duniani, hususan katika kusaka suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Ukraine na Urusi.

Imetolewa na: Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Stockholm - Sweden. 22 AGOSTI 2025

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...