MAHAKAMA Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam leo Novemba 28,2025 imetupilia mbali kesi ya madai ya kuidharau mahakama iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa Chadema akiwemo Makamu Mwenyekiti Bara, John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, pamoja na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu. Wajibu maombi wengine ni Rose Mayemba, Brenda Rupia, Gervas Lyenda, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya, Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Madai hayo yalitokana na kesi ya mgawanyo wa rasilimali kati ya Zanzibar na Bara, ambapo wadaiwa walidaiwa kukiuka amri ya mahakama iliyowazuia kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali za chama hadi kesi ya msingi itakapomalizika.
Katika uamuzi wake wa Novemba 28, 2025, Jaji Awamu Mbagwa alilitupilia mbali shauri hilo baada ya kukubaliana na pingamizi kwamba liliwasilishwa nje ya muda wa siku 60 kinyume na Sheria ya Ukomo wa Muda. Kiapo kinaonyesha matendo yanayolalamikiwa yalifanyika Juni 16–17, 2025, lakini shauri likafunguliwa Oktoba 3, 2025.
Jaji Mbagwa alisema sheria inaweka ukomo wa siku 60 na kuchelewa kunanyima mlalamikaji haki ya kusikilizwa. Kwa kukubaliana na pingamizi hilo, shauri limetupiliwa mbali kwa kuwa nje ya muda.
Katika kesi ya msingi mbele ya Jaji Hamidu Mwanga, wadai wanadai mgawanyo usio sawa wa mali za chama kati ya Zanzibar na Bara, ubaguzi wa kidini na kijinsia, na matamko yenye nia ya kuvuruga muungano. Wanaiomba mahakama itamke kuwa wadaiwa wamekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama, isitishe shughuli za kisiasa, na itoe zuio dhidi ya matumizi ya mali na fedha za chama.
Wadai pia waliwahi kuomba zuio la muda, ambalo lilitolewa Juni 10, 2025. Baadaye wakafungua shauri la kuidharau mahakama wakidai amri hiyo imekiukwa. Wajibu maombi waliwasilisha pingamizi wakidai mgongano wa masilahi, shauri kufunguliwa nje ya muda, na kwamba amri hiyo inawahusu wadaiwa kwenye kesi ya msingi pekee.
Pingamizi hilo lilisikilizwa Oktoba 28, 2025, sambamba na shauri la kuidharau mahakama. Katika kesi ya msingi, wadaiwa wameibua pingamizi jingine wakidai kuwa kesi yenye madai ya Kikatiba haipaswi kusikilizwa na jaji mmoja. Mahakama imeelekeza isikilizwe kwa njia ya maandishi.



.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...