MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu kuongezeka kwa kiwango cha joto nchini katika miezi ya hivi karibuni, hususan katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Kwa mujibu wa TMA, ongezeko hilo la joto limetokana na kusogea kwa Jua la Utosi sambamba na kupungua kwa mvua katika maeneo husika. Kawaida, vipindi vya Jua la Utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa Novemba wakati jua linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni), na hurudi tena Februari jua linapohamia kaskazini (Tropiki ya Kansa). Kipindi hiki huambatana na ongezeko la joto kutokana na eneo la uso wa dunia kuwa karibu zaidi na jua.
Katika mwezi huu wa Novemba 2025, hali hiyo imeonekana wazi katika vituo kadhaa vya hali ya hewa. Kufikia tarehe 27 Novemba 2025, kituo cha Moshi (Kilimanjaro) kilirekodi kiwango cha juu cha nyuzi joto 35.7°C mnamo 21 Novemba, ongezeko la nyuzi 4.2°C juu ya wastani wa muda mrefu wa Novemba. Kituo cha Ilonga (Morogoro) kilirekodi nyuzi joto 35.5°C Novemba 20 (ongezeko la 2.7°C), Morogoro Mjini nyuzi 34.5°C mnamo Novemba 26 (ongezeko la 2.3°C), huku Ibadakuli (Shinyanga) kikirekodi nyuzi 33.6°C Novemba 14 (ongezeko la 2.2°C). Dar es Salaam ilirekodi nyuzi joto 33.2°C mnamo 19 na 21 Novemba (ongezeko la 1.6°C).
Aidha, TMA imeeleza kuwa kuongezeka kwa unyevu angani, hususan kutokana na mvuke wa Bahari katika ukanda wa pwani na maeneo jirani, kumeongeza hisia ya joto kwa wananchi kuliko viwango halisi vinavyorekodiwa.
Hata hivyo, vipindi vya mvua vinatarajiwa kuanza kujitokeza katika maeneo mengi nchini mwanzoni mwa Desemba 2025, hatua ambayo inatarajiwa kusaidia kupunguza joto katika maeneo mengi ya misimu miwili ya mvua.
Mamlaka hiyo imetoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na TMA, sambamba na kupata ushauri wa kitaalamu katika sekta mbalimbali ili kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...