Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda na Naibu Waziri Mhe. Wanu Hafidh Ameir wameongoza Wataalamu wa Wizara na Kamati ya Program ya Samia Extended Scholarship DS/AI+ kujadili mwenendo wa program hiyo.

Program hiyo inalenga kufadhili vijana 50 wa Tanzania Bara na Zanzibar kusoma katika vyuo vikuu mahiri duniani, katika fani za Sayansi ya Data, Akili Bandia (Artificial Intelligence), na Sayansi Shirikishi kwa mwaka wa masomo 2025/2027.

Kwa sasa vijana hao wanaotarajiwa kunufaika na program hiyo, wanaendelea na maandalizi kwenye Kambi ya Maarifa katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) Arusha.

Katika majadiliano hayo Prof. Mkenda ameridhishwa na shughuli zinazotekelezwa na Kamati ya Programu hiyo inayongozwa na Prof. Makenya Maboko kwa kushirikiana na Viongozi na Wataalamu wa Wizara, ambapo amesema ni hatua nzuri katika kutekeleza azma ya Serikali ya kuandaa vijana wataalamu katika nyanja za sayansi teknolojia ili kuchochea maendeleo ya taifa.

Naye, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, amewahimiza wajumbe wa Kamati na Viongozi wa Wizara na Taasisi kuendelea kushirikiana kikamilifu na kutekeleza maagizo ya Waziri. Amesisitiza ufuatiliaji wa karibu kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na programu hiyo.

Mshauri wa Kamati ya Programu, ambaye pia ni Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, ameishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huu wa kimkakati. Ameahidi kuwa COSTECH itaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha utekelezaji wa programu unakwenda sambamba na matarajio ya Serikali.

Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa wakati akihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanapata nafasi za kusomea teknolojia za kisasa duniani ili kuimarisha uchumi wa taifa na kulinda mustakabali wa kizazi kijacho.

  

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...