Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda ametoa Wito kwa Umoja wa Wakuu wa Shule za msingi za Serikali na binafsi kwenda kuendelea kutekeleza mageuzi ya elimu huku kukiwa na kushauriana,kubaini changamoto na kuona namna ya kuzitatua.
Prof. Mkenda ametoa wito huo leo hii Jijini Dodoma Novemba 27,2025 wakati akifunga Mkutano wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara (TAPSHA).
Na kusisitiza kuwa mambo ya Elimu yanaanza huku chini kabisa katika Elimu ya awali Shule ya Msingi kwamba kukiharibika huku basi kunaharibika kote na tukijenga huku tunajenga kote.
"Kwahiyo natoa Wito twende tukatekeleze haya,tuendelee kushauriana na kuwasikiliza ninyi mniambie changamoto za huko mliko na nini kifanyike,kwani mambo ya elimu yanaanza huku kabisa elimu ya awali shule ya msingi,tukiharubu huku tunaharibu kote na tukijenga huku tunajenga kote".
Akizungumzia suala la mageuzi ya Elimu amesema kuwa ni muhimu sana kwa taifa, hivyo tunalazimika kuyatekeleza ili kuandaa vijana wetu kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kutumia fursa za teknolojia kuleta maendeleo katika nyanja mbalimbali Nchini.
"Ili kuwaandaa vijana kwa soko la ajira na kukabiliana na changamoto za utandawazi, tushirikiane kutekeleza mageuzi na tuwekeze kwenye sayansi na teknolojia".
Aidha ameongeza kuwa, katika kutekeleza Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Toleo la 2023, pamoja na mambo mengine Wizara inafanya maandalizi kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari hatua ya chini mwaka 2028.
Pamoja na hayo pia amesema Serikali inatambua mchango wa Umoja huo wa TAPSHA katika maendeleo ya elimu, hivyo amesisitiza chombo hicho kulinda familia ya walimu pamoja na kuwapongeza walimu wote Nchini kwa kazi nzuri wanaofanya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAPSHA Bi Rehema Ramole amesema kuwa moja ya malengo ya Umoja huo ni pamoja na kuwaunganisha Wakuu wa Shule zote za Msingi ili kuweza kushirikiana katika kutatua changamoto zinazoikabili Shule kitaaluma lakini pia kuelimisha Wanachama kwa kuandaa Semina za Uongozi,Mikutano na Warsha mbalimbali kwa lengo la kujadili na kusaidia katika kuboresha uwezo wa kitaaluma.
Akizungumzia mafanikio ya Umoja huo yaliyotekelezwa katika mwaka 2025 amesema ni pamoja na kupunguza idadi ya wanafunzi wasiomudu KKK na pia kufanikiwa kwa Miradi ya maendeleo kupitia Boost,Shule Bora na mingineyo.
Huu ni Mkutano wa 7 wa Umoja huo wa TAPSHA wenye Wanachama kutoka kote Halmashauri na Wilaya zote Nchini wapatao 20,889.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...