Na Saidi Lufune, Kilimanjaro
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), amewataka wahitimu wa chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, kuzingatia uadilifu, uzalendo na unyenyekevu wakati wa kuhudumia wananchi na kulinda rasilimali za wanyamapori ili kuongeza thamani katika maendeleo ya ukuaji wa sekta ya utalii kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla

Mhe. Chande ametoa wito huo mkoani Kilimanjaro wakati wa mahafali ya 61 ya chuo hicho kilichopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo amewasisitiza wahitimu hao kutumia vyema maarifa na taaluma ya elimu waliyopata kufanya kazi kwa weledi na ufanisi mkubwa katika kuisaidia jamii kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo kusaidia kutatua migogoro baina ya binadamu na Wanyamapori wakali na waharibifu

“Vyeti tu havitoshi, bali utekelezaji wa yale mliyojifunza na kufunzwa chuoni, hivyo nendeni kuyaonesha kwa vitendo huko mnapokwenda, kwa sababu cheti ni karatasi lakini maarifa mliyoyapata katika kutambua mnaishi vipi na jamii, nchi na rasilimali zinazokuzunguka hilo ndio muhimu kuliko zote” amesema Waziri Chande.

Aidha, Waziri Chande ametoa wito kwa chuo hicho katika kutanua wigo wa kada za masomo ikiwemo masomo ya muda mfupi katika fani za kuongoza watalii, huduma kwa wateja na udereva ili kutanua wigo kwa vijana kusomea masomo hayo mara baada ya kuhitimu elimu ya sekondari na msingi ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ili kusudi vijana hao wanapokuwa wanakwenda kuongoza watalii wawe na taaluma yao vizuri ili mtalii avutike mara nyingine kurudi na waweze kuelezea vizuru vivutio vyetu tulivyonavyo lakini pia waweze kuwa sehemu ya usalama wa vivutio vyetu na nchi yetu, hali itakayopelekea kuongeza kasi ya idadi wa watalii katika nchi yetu na kukuza pato la taifa” Amesema Mhe. Chande

Naye Mkuu wa chuo Prof. Julius Nyahongo, amesema kuwa udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2024/2025 umeongezeka kwa asililimia 10 ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi waliohitimu mwaka uliopita ikiwa ni mafanikio yanayoendana na mkakati wa Serikali wa kuongeza udahili wa wanafunzi wanaohitimu elimu za upili hapa nchini na kutoka mataifa mengine barani Afrika na duniani kote.

Kwa upande wake Prof. Yunus Mgaya, Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana ya Chuo amesema bodi ya chuo hicho imeidhinisha bajeti shilingi Bilion 16.3 kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za uendeshaji na miradi ya maendeleo ili kuimarisha mafunzo na tafiti katika chuo hicho ikiwemo ujenzi wa jiko, maliwato na madarasa katika eneo la mafunzo Loliondo mkoani Arusha, ujenzi wa maktaba, mabweni ya wanafunzi na ununuzi wa magari makubwa manne kwa ajili ya mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi

Jumla ya wanafunzi 649 wamehitimu Mafunzo yao katika chuo hicho kwa ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo ngazi ya shahada ya Uzamili katika programu za Usimamizi wa Utalii, Shahada ya Uzamili ya Uongozi katika Uhifadhi, Shahada ya Uzamili katika programu ya Ikolojia na Uhifadhi katika Bara la Afrika inayotolewa kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Manchester Metropolitan kilichopo nchini Uingereza na Chuo Cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...