AFISA Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) CPA.Nicodemus Mkama ameipongeza Bodi na Menejimenti ya Benki ya TCB kwa kutekeleza mikakati yenye lengo la kuboresha na kuimarisha utendaji wa benki hiyo.

Amesema maamuzi waliyofanya ya kutoa kwa umma hatifungani ya Stawi yamekuwa chachu katika kuongeza mtaji wa benki hiyo na ni hatua madhubuti ya kuongeza fursa za uwekezaji katika masoko ya mitaji na kuleta matokeo chanya kwenye uchumi wa nchi yetu.

CPA.Mkama ametoa pongezi hizo leo Desemba 3,2025 wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa Hatifungani ya Benki ya TCB (TCB STAWI BOND),katika soko la Hisa la Dar es Salaam.

Amesema hatifungani ya benki ya TCB (Stawi Bond) imeidhinishwa chini ya Sheria, Kanuni na Miongozo katika Masoko ya Mitaji na imepata mafanikio makubwakatika mauzo, na hatimaye leo hii inaorodheshwa rasmi katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.

“Kama tulivyoshuhudia mauzo ya hatifungani ya benki ya TCB (Stawi Bond) yamepata mafanikio ya asilimia 281, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 140.24 kimepatikana, ikilinganishwa na shilingi bilioni 50 zilizotarajiwa.

“Hatua hii inaiwezesha Benki ya TCB kuongeza ukwasi na kuimarisha kiwango cha mtaji.Ongezeko hili la ukwasi na mtaji linatarajiwa kuiwezesha benki ya TCB kuongeza ufanisi zaidi wa kutoa huduma za kibenki na kufikia makundi mengi zaidi ya wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.”

CPA.Mkama amesema Benki ya TCB imeweka historia ya kuwa benki ya kwanza (1) inayomilikiwa na Serikali kwa hisa nyingi kuuza hatifungani kwa umma na kupata mafanikio makubwa, na hatimaye leo hii hatifungani hii inaorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Ameongeza hatua hiyo inaweka msingi imara na inafungua milango kwa taasisi zingine za Serikali nasekta binafsi ambazo zinaonyesha nia ya kutumia fursa katika masoko ya mitaji kupata fedha za kuendesha biashara na kugharamia miradi ya maendeleo.

Aidha, hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Serikali wa Njia Mbadala za Kugharamia Miradi ya Maendeleo uliowekwa kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli na miradi ya maendeleo katika sekta ya umma na binafsi.

“Napenda kuufahamisha umma kuwa kati ya wawekezaji waliowekeza kwenye hatifungani ya benki ya TCB, asilimia 96.7 ni wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 3.3 ni Kampuni na Taasisi.Aidha, asilimia 99.6 ni wawekezaji wa ndani yaani Local Investors na asilimia 0.4 ni wawekezaji wa kigeni.”

Akieleza zaidi amesema kuorodheshwa kwa hatifungani ya benki ya TCB kunaongeza thamani ya uwekezaji katika Hatifungani za Kampuni na Taasisi kwa asilimia 8.2 na kufikia shilingi trilioni 1.8, kutoka shilingi trilioni 1.7.

Amesema ushiriki huo mkubwa wa wawekezaji mmoja mmoja wa ndani ni hatua muhimu katika kuongeza ukwasi katika soko na utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Kifedha wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wananchi kwenye sekta rasmi ya fedha.

Amesisitiza kuorodheshwa kwa TCB Stawi Bond kunatoa fursa kwa wawekezaji kuuza hatifungani zao pale watakapohitaji fedha kwa ajili ya matumizi mengine, na kuwapatia fursa wawekezaji wapya kununua hatifungani hizi.

Aidha, amesema uorodheshwaji wa hatifungani katika Soko la Hisa unawawezesha wawekezaji kujua thamani halisi ya hatifungani zao (Price Discovery); ambapo wawekazaji hao watapata faida ya uwekezaji wao (coupon payments).

Pia, Kuorodheshwaji wa hatifungani katika soko la hisa kunaimarisha utawala bora katika uendeshaji wa kampuni; na kumuwezesha mwekezaji kuwa na anuwai na hivyo hupunguza athari za uwekezaji (Diversification).

“Hivyo, tuna kila sababu ya kuipongeza benki ya TCB pamoja na taasisi na wataalamu wote walioshiriki katika kuwezesha mafanikio haya. Mafanikio haya ni uthibitisho wa imani ya waliyonayo wawekezaji kwa benki ya TCB na masoko ya mitaji nchini.

Aidha, mafanikio haya ni matokeo ya mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kiutendaji yanayotolewa na Serikali katika masoko ya mitaji.








Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...