Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiwezesha Manispaa ya Moshi kupata ongezeko la bajeti ya shilingi bilioni 4 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 — hatua anayoitaja kuwa ni uwekezaji mkubwa wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kasi ya maendeleo ya Moshi.

Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mnzava amesema ongezeko hilo linaonesha dhamira ya Serikali kuimarisha huduma za kijamii na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika manispaa hiyo.

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Manispaa ya Moshi ilikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 52, huku bajeti mpya ya 2025/2026 ikifikia bilioni 56, na hivyo kuongeza zaidi ya bilioni 4 ambazo zinatarajiwa kuelekezwa kwenye miradi ya miundombinu, afya, elimu na usimamizi wa huduma za jamii.

Mnzava amesema bajeti hiyo mpya itaiwezesha manispaa kufungua fursa zaidi za maendeleo na kuongeza ufanisi wa utendaji katika sekta mbalimbali.

“Ongezeko hili litatusaidia kusukuma miradi ya kijamii kwa kasi, kuboresha huduma, na kuhakikisha wananchi wa Moshi wananufaika moja kwa moja na uwekezaji huu wa Serikali,” amesema Mnzava.

Amesisitiza kuwa uongozi wa manispaa, wakuu wa idara na wataalamu wanapaswa kusimamia bajeti hiyo kwa uadilifu, ili iweze kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi wa kisiasa, wakuu wa idara, taasisi za umma na viongozi wa dini, ambapo masuala mbalimbali ya maendeleo ya wilaya yalijadiliwa, ikiwemo utekelezaji wa miradi inayotarajiwa kusimamiwa kupitia ongezeko hilo la fedha.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...