Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) ina adhimisha Siku ya Ushindani Duniani kwa kutoa wito kwa wafanyabiashara na watumiaji wa huduma au bidhaa kushiriki kikamilifu katika kujenga mazingira ya ushindani yenye haki, uwazi na uadilifu ili kukuza uchumi wa Taifa.Maadhimisho ya Siku ya Ushindani Duniani hufanyika kila mwaka ya Desemba 5 na kuratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD). Maadhimisho hayo hufanyika Kitaifa kupitia Tume ya Ushindani.
Amesema kuwa shughuli za maadhimisho kuanza Desemba moja kwa kutanguliwa kwa utoaji wa elimu kwa wadau, makongamano, semina, mijadala ya wataalam, pamoja na kampeni za uhamasishaji ikilenga kufikisha ujumbe kwa makundi mbalimbali ya wananchi na ambapo Desemba 5 ni kilele na ufungaji na mgeni rasmi atakuwa ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga (Mb).
Ngasongwa amesema kuwa mwaka huu kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Ushindani ni "Akili Mnemba, Walaji na Sera Ushindani."
Amesema kuwa ushindani bora ni nguzo muhimu inayokuza ubunifu, kuongeza ubora wa bidhaa na huduma, na kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa mwananchi.
Amesema maadhimisho ya mwaka huu yameweka mkazo katika elimu kwa umma, hatua zinazolenga kupunguza vitendo vya upotoshaji wa bei, mikataba isiyo ya haki, na makubaliano ya pamoja ya wafanyabiashara yanayoweza kudhoofisha ushindani.
“FCC inaendelea kuhakikisha masoko yanatenda kazi kwa uhuru na haki. Tunatoa elimu kwa wafanyabiashara kufuata sheria pamoja na kuwaelimisha watumiaji kutambua haki zao na namna ya kuripoti ukiukwaji,” alisema Ngasongwa
Ngasongwa amesema kauli mbiu ya maadhimisho imekuja kwa wakati mwafaka ikiwa ni sehemu ya maagizo Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kutaka matumizi ya Mifumo ya Tehama ya kusomana katika kutoa huduma kwa jamii.
Aidha, Tume imewahimiza wafanyabiashara kuzingatia Sheria ya Ushindani ya mwaka 2003, ili kuepuka adhabu zinazoweza kutokea kutokana na vitendo vya udanganyifu na ukiritimba wa upandishaji bei au ushushaji bei usio zingatia ushindani.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...