Dar es Salaam – Katika hafla ya Marketers Night Out iliyofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, aliwasilisha mada iliyoangazia kwa kina mchango wa programu ya Imbeju katika kubadilisha maisha ya wananchi, hasa wanawake na vijana, kupitia uwezeshaji wa kiuchumi na kukuza ujumuishi wa kifedha nchini.


Akizungumza mbele ya wataalamu wa masoko, viongozi wa taasisi, wajasiriamali na wadau wa maendeleo, Mwambapa alisema Imbeju ni zaidi ya mpango wa kutoa mikopo pekee bali ni programu jumuishi inayolenga kujenga msingi imara wa ujasiriamali. Alieleza kuwa programu hiyo imejengwa juu ya nguzo tatu kuu; elimu ya ujasiriamali na uongozi, upatikanaji wa mitaji rafiki, pamoja na uunganishaji wa wajasiriamali na masoko pamoja na huduma rasmi za kifedha.
 
“Kupitia mafunzo ya vitendo, washiriki huwezeshwa kuendesha biashara zao kwa ufanisi zaidi, kutumia fursa za teknolojia, kufuatilia mapato na faida kwa weledi na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji. mbinu hiyo imewezesha wajasiriamali wengi kuimarisha biashara zao na kuongeza ajira katika jamii”, alisema Mwambapa

Akizungumzia wanawake, Mwambapa alieleza kuwa wamekuwa walengwa muhimu wa programu kwani ndio mhimili wa ustawi wa familia na jamii. Wanawake wengi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za mtaji na elimu ya ujasiriamali sasa wameweza kuanzisha au kupanua biashara zao kupitia Imbeju, jambo lililosababisha kuongezeka kwa uzalishaji, kuboreshwa kwa kipato cha kaya na kuinuka kwa hali ya maisha ya familia zao. Alisisitiza kuwa uwekezaji kwa mwanamke mmoja hupelekea kuleta mafanikio kwa kizazi kizima.

Kwa upande wa vijana, alisema programu hiyo imekuwa chachu ya kubadilisha fikra bunifu kuwa miradi halisi katika maeneo ya teknolojia, kilimo-biashara, sanaa na biashara mtandao. Kupitia ushauri wa kitaalmu, mafunzo na ufadhili wa mawazo bunifu, vijana wengi wamepata uwezo wa kuzifikisha bidhaa zao katika masoko mengi zaidi kupitia majukwaa ya kidijitali, hivyo kuongeza ushindani na kupanua wigo wa biashara zao.
 
Mwambapa pia aligusia mchango wa Imbeju katika kukuza ujumuishi wa kifedha nchini kwa kuwawezesha wananchi waliokuwa nje ya mfumo rasmi wa benki kufungua akaunti, kujiwekea akiba, kukopa na kufanya miamala kwa urahisi zaidi baada ya kupata elimu ya kifedha. Kupitia ushirikiano wa CRDB Bank Foundation na Benki ya CRDB, huduma hizi sasa zimefika hata maeneo ya vijijini ambako upatikanaji wa huduma za kifedha ulikuwa mdogo awali.

Alisema hatua hiyo imeimarisha uthabiti wa biashara ndogondogo, kuongeza uwezo wa kujitegemea kwa wananchi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akihitimisha mada yake, Mwambapa alitoa wito kwa wadau wote kuendelea kuwekeza katika mipango inayowawezesha wanawake na vijana, akisisitiza kuwa mafanikio ya Imbeju ni ushahidi kuwa uwekezaji katika watu ndiyo msingi wa kujenga uchumi jumuishi, thabiti na wenye tija kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...