Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amewasihi watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia dhamana kubwa waliyopewa ya kusimamia suala la Mazingira na Muungano hapa nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Dodoma. Amewataka kutambua na kuchukulia kwa uzito suala la uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwani linabeba mustakabali wa vizazi vya sasa na baadaye.
Aidha amewataka kuwa na utaratibu wa upimaji wa malengo yaliyowekwa katika Wizara hiyo ikiwemo upandaji wa miti ili kuhakikisha utekelezaji wa mipango na malengo ya uhifadhi mazingira yanakuwa na matokeo mazuri na yenye manufaa.
Makamu wa Rais, amesema ni lazima Wizara hiyo kutambua umuhimu wa suala la Muungano kwa kuhakikisha elimu inatolewa vya kutosha kwa wananchi hususani vijana kwa kuhusianisha maendeleo na mafanikio ya Taifa yanategemea uimara wa Muungano.
Ameongeza kwamba, kutokana na idadi kubwa ya wananchi waliozaliwa baada ya Muungano mwaka 1964, ni vema kutoa elimu ya kuwafahamisha umuhimu na uzuri wa Muungano ili kuweza kuendeleza yale ya Serikali zilizopita na kuwa na Taifa zuri zaidi kwenda mbele.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Wizara hiyo kujipanga kuhakikisha inatekeleza hapa nchini, maazimio na mipango ya kulinda mazingira yanayofikiwa katika mikutano ya kimataifa ambayo Tanzania inashiriki.
Vilevile, Makamu wa Rais amewataka watumishi wa Wizara hiyo kuzingatia ahadi za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizotoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, kwa kubainisha yale yanayohusu Wizara hiyo na yatekelezwe kwa ufanisi.
Makamu wa Rais amewasihi watumishi hao, kuisoma na kuelewa vema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kubaini maeneo ambayo Wizara inahusika zaidi na kuhakikisha yanatekelezwa. Pia amewaagiza kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi 2025 - 2030 na kutekelezaa yale ambayo Wizara inahusika moja kwa moja.
Makamu wa Rais amewahimiza kuzingatia mafunzo kazini ili kuweza kuenda sambamba na mabadiliko yanayojitokeza pamoja na kufanya kazi kwa bidii na nidhamu na kuwa mfano mzuri katika Serikali.
Awali Makamu wa Rais, alitembelea na kukagua jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira linalojengwa katika Mji wa Serikali Mtumba mkoani Dodoma, na kupongeza hatua kubwa iliyofikiwa katika ujenzi huo na kuwasihi wakandarasi kuhakikisha wanatimiza ahadi ya kukamilisha jengo hilo ifikapo mwezi Machi 2026.











Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...