Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kimekutana na Balozi wa Cuba nchini Tanzania kwa lengo la kujadili na kuimarisha ushirikiano kati ya SUA na Chuo Kikuu cha Artemisa cha Jamhuri ya Cuba. Ushirikiano huo unalenga kutekeleza miradi na tafiti mbalimbali, hususan zinazohusiana na maendeleo ya sekta ya kilimo ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Kampasi ya Edward Moringe, Morogoro, Prof. Samwel Kabote, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo amesema ushirikiano huo utahusisha kufanya tafiti za pamoja, kubadilishana wataalamu na kuandaa andiko la namna bora ya kushirikiana.
Aidha, tayari baadhi ya wataalamu wa lugha kutoka Cuba wameanza kutoa mafunzo ya lugha za kigeni chuoni hapo.
Prof. Kabote ameongeza kuwa matarajio ya ushirikiano huo ni kuboresha na kuendeleza sekta ya elimu nchini Tanzania na kimataifa, kufuatia makubaliano yaliyosainiwa mwaka 2024 kati ya vyuo hivyo viwili.
Kwa upande wao, wataalamu wa lugha kutoka Cuba, Bi Yusimi Vigoa na Bw. Razaro Nochea. Wameeleza kufurahishwa na mapokezi mazuri waliyoyapata SUA na kujiona kama mabalozi wa nchi yao chuoni hapo.
Wameonyesha utayari wa kushirikiana kikamilifu katika ufundishaji na kuiomba SUA kuendeleza ushirikiano, hasa panapojitokeza changamoto katika mchakato wa kutoa mafunzo.
Ushirikiano huu kati ya SUA na Chuo Kikuu cha Artemisa unatarajiwa kuleta maendeleo chanya katika sekta ya elimu na kilimo, sambamba na kuchangia ukuaji wa taaluma, maarifa na utafiti utakowanufaisha wananchi wa Tanzania na Cuba.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...