Makumbusho ya Taifa la Tanzania yameibuka mshindi wa Tuzo ya Huduma Bora ya Uhifadhi wa Utamaduni na Urithi wa Taifa kwa Mwaka 2025 katika Tuzo za Ubunifu katika Utumishi wa Umma 2025, kwenye hafla iliyofanyika jana, tarehe 16 Desemba 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo ilitolewa na Bodi ya Tuzo za Ubunifu katika Sekta ya Umma kwa lengo la kutambua jitihada bunifu na endelevu za Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa kitamaduni na kihistoria wa Taifa, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma za umma zinazomlenga mwananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Bw. Hamis Suleiman Mwalimu, alisema kuwa tuzo hizo ni chachu ya kuhamasisha ubunifu na maboresho endelevu katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi za umma.

“Tuzo hizi ni hatua muhimu ya kuhamasisha ubunifu katika utumishi wa umma na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa njia zenye ufanisi, uwajibikaji na tija,” alisema Bw. Mwalimu.

Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya Tuzo za Ubunifu katika Sekta ya Umma, Bw. Steven Mkomwa, alisema kuwa tuzo hizo zinafanyika kwa mara ya kwanza nchini zikiwa na lengo la kuhamasisha taasisi za umma kuendeleza ubunifu na kuboresha huduma kwa wananchi.

“Tunatarajia tuzo hizi zitakuwa chachu ya mabadiliko chanya katika utoaji wa huduma za umma na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa,” alisema Bw. Mkomwa.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Bw. James Mganga, aliwashukuru waandaaji wa tuzo hizo na kueleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya juhudi za pamoja za watumishi wa Makumbusho ya Taifa katika kuhifadhi na kuenzi urithi wa Taifa kwa kutumia mbinu bunifu na za kisasa.

“Tuzo hii ni motisha kubwa kwetu kuendelea kuboresha huduma za uhifadhi wa utamaduni na urithi wa Taifa, sambamba na kuimarisha ushirikiano na jamii katika kulinda historia na utambulisho wa nchi yetu kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema Bw. Mganga.

Makumbusho ya Taifa la Tanzania yameendelea kuwa taasisi kinara katika uhifadhi wa utamaduni na urithi wa Taifa kwa kuanzisha programu bunifu za elimu, tafiti, maonesho ya kihistoria na ushirikishwaji wa jamii, hatua inayochangia kukuza utalii wa utamaduni na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa urithi wa Taifa.

Tuzo za Ubunifu katika Utumishi wa Umma 2025 zinalenga kutambua na kuthamini ubora, ubunifu na weledi katika utoaji wa huduma za umma, kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, utawala bora na maboresho endelevu katika taasisi za umma nchini.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...