Na Pamela Mollel, Arusha
Jamii ya wauguzi, madaktari na wananchi waliopo katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru wamepata faraja na motisha baada ya mfanyabiashara na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hokimart Group Limited, Nathan Kimaro, kutoa msaada wa kijamii uliolenga kuthamini mchango wa watoa huduma za afya.
Kupitia tukio hilo, Nathan aligawa vitu mbalimbali ikiwemo mafuta ya kupikia, sabuni, pampasi za watoto pamoja na kushiriki chakula cha pamoja na wauguzi na wananchi, hatua iliyodhihirisha moyo wa kujitolea na kugusa maisha ya jamii.
Akizungumza katika tukio hilo, Nathan alisema kada ya afya ni mhimili muhimu wa maisha ya binadamu kwani hugusa maisha ya watu wengi bila kutambuliwa, huku ikibeba majukumu mazito ya kuokoa maisha ya wagonjwa mchana na usiku.
“Mtu akiwa anaumwa husema aitwe daktari, lakini akipona humshukuru Mungu"
Aidha aliongeza kuwa kuna mikono mingi isiyoonekana inayohakikisha maisha yanaendelea
Aliongeza kuwa taaluma ya tiba hupimwa kwa kukosa usingizi, kufanya maamuzi magumu na mikono isiyochoka, huku wahudumu wa afya wakiendelea kutoa huduma hata wakati wa sikukuu, majanga na nyakati ngumu.
Aidha, alisema baadhi ya wagonjwa hawatambui hata majina ya wauguzi au madaktari waliowahudumia, huku wahudumu hao wakifanya kazi bila tuzo wala sifa, bali kwa kujitoa kwa dhati ili kuokoa maisha ya wengine.
Katika hatua nyingine, Nathan aliomba uongozi wa hospitali hiyo, akiwemo Matron Simphorosa Silalye na Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, kumpa eneo la Bustani ya Matumaini ili aweze kulitengeneza kwa lengo la kuwapa wagonjwa faraja na matumaini ya kupona changamoto zao za kiafya.
Pia aliwahimiza wananchi waliopona kurejea hospitalini kutoa shukrani kwa wauguzi na madaktari.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Godson Mollel, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya afya katika Hospitali ya Mount Meru, akisema hatua hiyo imeongeza ubora wa huduma kwa wananchi.
Naye Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Dk. Abel Ndago, alimpongeza Nathan kwa mchango wake kwa jamii, akisema msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwemo mafuta ya kupikia, sabuni na pampasi za watoto umeleta faraja kwa wauguzi na familia zao.
Baadhi ya wauguzi akiwemo Maryam Ismail na Samweli John, walieleza shukrani zao wakisema msaada huo umeongeza ari ya kazi na kuwafanya wajisikie kuthaminiwa na jamii.
Msaada huo umetolewa ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 27 ya kuzaliwa kwa Nathan Kimaro,akiamua kuisherehekea siku hiyo kwa kugusa maisha ya wengine na kuacha alama chanya kwa jamii.


.jpeg)







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...