Mwamvua Mwinyi, Kisarawe Disemba 2,2025
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameagiza mafunzo ya kuwajengea weledi maofisa usafirishaji (bodaboda) kuhusu usalama barabarani na sheria za usafirishaji kutolewa katika mkoa mzima.
Aidha, amezitaka mamlaka husika, ikiwemo Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuhakikisha wahitimu wanapatiwa leseni mara baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo.
Kunenge alitoa agizo hilo , wakati akizindua mafunzo hayo kwa maafisa usafirishaji wa Wilaya ya Kisarawe, yanayofanyika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya.
Alisisitiza umuhimu wa maafisa hao kuwa wazalendo, kulinda amani ya nchi na kuwa mfano bora katika utendaji wao ili kuipa heshima Serikali na kumuenzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Nyinyi ni wasomi na wadau wakubwa wa uchumi katika nchi yetu, kwa mujibu wa Katiba, kulinda usalama wa nchi ni wajibu wa kila raia, "Uzalendo ni kujiuliza umeifanyia nini nchi yako, siyo imekufanyia nini,” alieleza Kunenge.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, ACP Salim Morcase, alitoa rai kwa maofisa usafirishaji kuunda vikundi na kuvisajili mara baada ya kupata leseni ili kukidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya asilimia 10.
Aliwapongeza kwa ushirikiano wao na kuwataka kuwa mabalozi wa amani pamoja na kuepuka matumizi mabaya ya mitandao.
Naye Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Pwani, SSP Edson Mwakihaba, aliwahakikishia washiriki kuwa leseni zao zitatolewa kwa haraka mara watakapokamilisha mafunzo.Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa awamu ambapo Awamu ya kwanza ilifanyika Novemba 22, 2025 na kushirikisha maifisa usafirishaji 228, huku awamu ya pili ikihusisha washiriki 250.




.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...