Katavi, Desemba 02, 2025

Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Andrew Mwalugaja amewakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa katika Sekta ya Madini, akibainisha kuwa mkoa huo umebahatika kuwa na rasilimali za madini ikiwemo dhahabu, shaba, risasi, fedha, nikeli, manganese na madini ya ujenzi.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Mhandisi Mwalugaja amesema ofisi yake imeendelea kuongeza ushiriki katika Sekta ya Madini kupitia utoaji leseni mpya, ikiwemo leseni tatu za utafiti katika mwaka wa fedha 2025/2026 kati ya Julai na Oktoba 2025 katika Wilaya za Mpanda, Tanganyika na Mlele, leseni 19 za uchimbaji wa kati, pamoja na leseni 290 za uchimbaji mdogo.

Ameongeza kuwa utoaji wa leseni za biashara ya madini nao umeimarika, ambapo mwaka wa fedha 2024/2025 jumla ya leseni 107 zilitolewa, 35 za biashara kubwa ya madini na 72 za biashara ndogo ya madini. Tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026 mapema Julai hadi Oktoba, leseni 82 za biashara ya madini zimetolewa zinazojumuisha leseni kubwa 34 na ndogo 48.

Amesema Serikali imeanzisha masoko mawili ya madini katika Manispaa ya Mpanda na eneo la Karema ili kuhakikisha wachimbaji wanapata soko la uhakika, huku mazingira ya uwekezaji yakiendelea kuimarika kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa katika kuongeza usalama na mifumo rafiki kwa wawekezaji.

Ameeleza kuwa Sekta ya Madini imeendelea kuleta mafanikio makubwa, hususan katika ongezeko la maduhuli ya Serikali kutoka Shilingi bilioni 1.16 mwaka 2017/2018 hadi Shilingi bilioni 9.26 mwaka 2024/2025. Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2025 pekee, Shilingi bilioni 3.80 tayari zimekusanywa sawa na asilimia 38 ya lengo la mwaka la Shilingi bilioni 10.

Wadau wa madini katika mkoa huo wamepongeza juhudi za Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji, wakibainisha kuwa maboresho ya miundombinu, utatuzi wa changamoto kwa haraka na upatikanaji wa huduma za kiserikali kwa wakati kumeongeza ufanisi katika shughuli zao. 

Wamesema kuwa uratibu mzuri kati ya Serikali na wachimbaji umefanya shughuli nyingi kuwa na uwazi zaidi, hali inayowavutia vijana wengi kuingia sekta hiyo kwa kuiona kuwa ya uhakika na salama.

Kwa niaba ya wadau, Joseph Lazaro, mmiliki wa leseni ya uchimbaji mdogo wa madini na mmoja wa Wakurugenzi wa Jiuxing Tanzania Mining Company amesema ushirikiano wao na wawekezaji kutoka China umeongeza uzalishaji wa madini, kutoa ajira kwa vijana 500 wa Mpanda na kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi. 

Amesema kuwa utaratibu wa Serikali kutoa ushauri wa kitaalamu, kutoa vibali kwa wakati na kutoa mwongozo wa kiufundi umesaidia wachimbaji wengi kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kujiamini.

Naye Adamu Mungwira kutoka kampuni hiyo amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uzalishaji wa makinikia ya shaba (froth flotation) yameboresha usalama, kupunguza athari za kimazingira na kuongeza viwango vya uzalishaji. 

Amefafanua kuwa teknolojia hiyo imewapa uwezo wa kuchakata kiasi kikubwa cha mawe ya madini kwa muda mfupi, jambo ambalo limeongeza tija na kuleta matokeo chanya kwa wachimbaji wa eneo hilo, hususan vijana wanaojifunza mbinu za uchimbaji wa kisasa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...