Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 22, 2025.


Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha malezi bora ya watoto na kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na makundi maalum, ikisisitiza kuwa ulinzi wa mtoto ni jukumu la familia, jamii na Taifa kwa ujumla. Hatua hizo ni sehemu ya utekelezaji wa sera na programu za kijamii zinazolenga kujenga jamii yenye maadili, usawa na ustawi wa kudumu.

Akizungumza leo Desemba 22, 2025 jijini Dar es Salaam  wakati wa kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo na fursa kwa makundi maalum kwa mwaka wa fedha 2025/26, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu ya malezi na makuzi bora ya watoto ili kuwajenga watoto kuwa raia wenye maadili mema na uzalendo.

Dkt. Gwajima amesema kupitia Mwongozo wa Wajibu wa Wazazi na Walezi katika Malezi na Matunzo ya Watoto na Familia, Serikali imeendelea kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa baba na mama katika malezi ya watoto, ili kuhakikisha ukuaji timilifu wa mtoto kimwili, kiakili na kisaikolojia.

Ameeleza kuwa Serikali pia inatekeleza Programu ya Malezi ya Vijana Balehe (Furaha Teen) katika mikoa ya Songwe na Mbeya, ambayo imelenga kuwajengea wazazi uwezo wa kuwalea na kuwaongoza vijana wao katika kipindi cha balehe, hatua inayosaidia kuzuia mmomonyoko wa maadili na tabia hatarishi miongoni mwa vijana.

Katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili, Waziri Gwajima amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza kampeni za kijamii zinazolenga kuelimisha jamii, kukemea na kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto. Kupitia kampeni hizo, matukio ya ukatili yamekuwa yakiripotiwa na kushughulikiwa kwa haraka zaidi.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta mbalimbali wakiwemo maafisa ustawi wa jamii, walimu wa unasihi, wahudumu wa afya na polisi jamii, ili kuhakikisha huduma za ulinzi, ushauri nasaha na msaada wa kisaikolojia zinapatikana kwa waathirika wa ukatili katika ngazi ya jamii.

Aidha, Serikali imeendelea kusajili na kufuatilia Makao ya Watoto na Vituo vya Kulelea Watoto Wadogo Mchana (Day Care Centers) ili kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yenye staha. Dkt. Gwajima amehimiza jamii kuanzisha na kutumia vituo hivyo kama sehemu ya kuboresha malezi na ulinzi wa watoto.

Waziri Gwajima pia ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto na mapambano dhidi ya ukatili, akisisitiza kuwa mtoto aliyelelewa katika mazingira salama na yenye upendo ndiye msingi wa Taifa lenye amani, maendeleo na ustawi wa kijamii.

Matukio mbalimbali.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...