Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Revocatus Bugumba ambaye ni Muhifadhi Mkuu mambo ya kale amewasihi Watafiti mbalimbali nchini kutafuta namna bora ya kuziwasilisha taarifa za kihistoria kwa kutumia njia mbalimbali katika jamii iwe katika Vitabu au kuandaa maonesho kwani historia ndio msingi,Urithi na Alama ya Taifa letu na kumekuwa na kufifia kwa watu kuzifahamu taarifa mbalimbali za kistoria.
Bugumba ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Desemba 16,2025 wakati akifungua Mkutano wa 9 wa Mwaka wa Chama cha Wanahistoria wa Tanzania (HAT) ambapo amemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa.
Na kusema kuwa Watafiti wanafanya tafiti mbalimbali kila mwaka tangia wakiwa wanafunzi mpaka wanapokuwa Wahadhiri kwa tafiti za masomo yao na vumbuzi hivyo ni vyema wakafanya kwaajili jamii kujua historia.
"Wito wangu kwamba kulingana na mabadiliko ya kiteknolojia na kufifia kwa watu kuzifahamu taarifa mbalimbali za kistoria ambazo tunajua ndio msingi wa nchi hii,ndio Urithi wa Taifa letu na Alama ya Taifa letu, wanapaswa kwa namna yeyote kutafuta namna bora ya kuziwasilisha kwa njia mbalimbali katika jamii iwe ni kwa maonesho,kuandika vitabu na watoto kuweza kusoma historia au gunduzi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini wakaelewa historia ya tulipotola".
Aidha amesema kuwa tamaduni zilizopo katika jamii zihamasishwe, na Wananchi waendelee kuzitunza na pia wasitupe vitu vya zamani na wasisite kwenda kupata ushauri Makumbusho ya Taifa kuhusu masuala ya uhifadhi wa mali kale.
Pia amesema Sheria yao ya mambo ya kale pamoja na marekebisho yake imeruhusu uandaaji wa Makumbusho binafsi hivyo watu wanaweza kushiriki kuandaa Makumbusho binafsi iwe ya familia,ukoo,kijiji,kata au hata tarafa.
Kwa upande wake Rais wa Chama cha Historia Tanzania Prof Maxmillian Chubila amesema Chama hicho kilianzishwa kwa malengo mahsusi ya kukusanya na kusambaza taaluma zote zinazohusiana na historia na wanafanya hivyo kwa historia ya Tanzania na Chama kuwa miongoni mwa vyama vikongwe Tanzania.
Na kuongeza kuwa wamekuwa wakifanya makongamano ya kitaaluma kila mwaka na mwaka huu wameongozwa na mada inayosema kuangalia historia kama urithi wa Taifa,kwasababu wanatambua umuhimu ambao historia inao katika maendeleo ya nchi yeyote duniani.
Kwani jamii bila historia inakuwa jamii mfu hivyo ili jamii ionekane kuwa ipo ni lazima iwe na historia na baada ya kutambua hilo sasa Tanzania ina somo la Historia ya Tanzania na Maadili litakalo saidia vijana kutambua umuhimu wa uzalendo.
Naye Dkt Mkubwa Ali ambaye ni Mkuu wa Idara ya Historia na Makumbusho akiuwakilisha Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma amesema jitihada wanazochukua kama idara ya historia ili kuendeleza historia ni kujikita katika tafiti tofauti na kuwatembeza wanafunzi sehemu mbalimbali za kihistoria ili kuendeleza somo la historia na kujua historia yenyewe.
Chama hiki kilianzishwa mwaka 1964 na mlezi wa kwanza alikuwa ni Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutambua umuhimu wa historia akakubali kuwa mlezi.



.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...