Na Mwandishi Wetu
KATIKA hatua inayochochea mapinduzi ya usafiri rafiki kwa mazingira, kampuni ya magari ya China, Harmony Auto, imezindua rasmi duka lake la magari ya BYD aina ya Pickup nchini Tanzania, likilenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza uchafuzi wa mazingira unaotokana na magari yanayotumia mafuta pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwakilishi wa Mauzo wa Harmony Auto, Khatibu Hamis Hussein, amesema kuwa kuletwa kwa magari ya BYD yenye teknolojia ya Plug-in Hybrid ni mchango muhimu katika juhudi za kulinda mazingira kwa kupunguza hewa chafu (carbon emissions) inayochangia mabadiliko ya tabianchi.

“Magari haya yana uwezo wa kutumia umeme pekee kwa umbali wa zaidi ya kilomita 100 baada ya kuchaji kwa saa mbili, jambo linalopunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya mafuta na uchafuzi wa hewa, hasa katika miji mikubwa,” amesema Hussein.

Ameongeza kuwa kwa kutumia teknolojia ya kuchaji kwa kasi ya juu (DC fast charging), betri inaweza kujaa ndani ya dakika 30.

Showroom hiyo, iliyopo barabara ya Nyerere karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, inauza magari mbalimbali ya Plug-in Hybrid yanayochanganya matumizi ya umeme na mafuta, yakilenga kutoa suluhisho la usafiri endelevu kwa Watanzania.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkazi wa Harmony Auto wa Kanda ya Afrika na Ukanda wa Mashariki, uzinduzi wa duka hilo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuunga mkono ajenda ya Afrika ya matumizi ya nishati mbadala na maendeleo ya uchumi wa kijani.

“Tunapanua uwekezaji wetu barani Afrika kwa lengo la kuhakikisha teknolojia safi ya usafiri inapatikana kwa urahisi. Mbali na matawi yetu Afrika Kusini, Msumbiji na Kenya, sasa Tanzania ni sehemu ya mkakati huu wa kulinda mazingira,” amesema.

Amefichua pia mipango ya kuanzisha kiwanda cha kutengeneza magari Afrika Kusini na kituo cha kuunganisha magari hapa Tanzania, hatua itakayopunguza gharama na kuongeza ufanisi wa magari kulingana na mazingira ya ndani.

Ameongeza kuwa ingawa kwa sasa magari hayo yanatumia mfumo wa lugha ya Kiingereza, mipango ipo ya kuingiza lugha ya Kiswahili ili kuwafanya watumiaji wengi zaidi wa ndani kunufaika na teknolojia hiyo safi.
Kwa upande wake,  Meneja wa Tawi wa Harmony Auto, Lee Ming alisema kampuni hiyo inatoa magari mbalimbali yakiwemo pick-up za double cabin aina ya BYD Shark 6, mini SUV na magari ya kifahari, yote yakizingatia teknolojia ya kisasa inayolenga matumizi bora ya nishati na uhifadhi wa mazingira.

Kampuni ya BYD inajulikana kimataifa kwa ubunifu wa betri salama, zenye uimara na ufanisi mkubwa, teknolojia inayosaidia kupunguza utegemezi wa mafuta na kulinda afya ya binadamu pamoja na mazingira.

Mmoja wa wateja wa kwanza, Faraji Shemsanga kutoka Morogoro, amesema uamuzi wake wa kununua BYD Shark 6 ulitokana na dhamira yake ya kuchangia utunzaji wa mazingira. “Ni gari linalookoa mafuta na pia ni rafiki kwa mazingira. Hii ni njia yangu ya kushiriki kulinda dunia yetu,” amesema.

Uzinduzi wa Harmony Auto na BYD nchini Tanzania unatarajiwa kuimarisha juhudi za kitaifa za kupunguza uchafuzi wa mazingira, kukuza matumizi ya nishati safi na kuhimiza kizazi kipya cha usafiri endelevu nchini.



Matukio mbalimbali katika uzinduzi huo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...