Accra, Ghana
Tume ya Madini Tanzania imefanya ziara ya kikazi kwa Bodi ya Dhahabu ya Ghana (Ghana Gold Board – GoldBod) jijini Accra, ikiwa na lengo la kujifunza kwa vitendo namna taasisi hiyo ya kipekee imefanikiwa kubadilisha taswira ya biashara ya dhahabu nchini Ghana na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Ziara hiyo ya mafunzo ya kubadilishana uzoefu (peer learning) imebaini kuwa GoldBod imeweka mifumo madhubuti ya kuwasimamia wachimbaji wadogo na kuwajumuisha katika mfumo rasmi wa biashara ya dhahabu.
Hatua hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vitendo vya udanganyifu na utoroshaji wa dhahabu, kuongeza mapato ya serikali na fedha za kigeni, pamoja na kuimarisha akiba ya dhahabu ya Benki ya Ghana.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa GoldBod, Profesa Richard Nunekpeku, amesema kwa kipindi kirefu wachimbaji wadogo walikuwa nje ya mfumo rasmi, hali iliyosababisha upotevu mkubwa wa mapatato kwa serikali.
Amesema kuanzishwa kwa GoldBod kumewezesha dhahabu yote inayozalishwa kukusanywa na kufanyiwa biashara kwa njia halali, hivyo kuchangia mapato ya taifa, kuongeza akiba ya dhahabu ya Benki ya Ghana na kudumisha uthabiti wa thamani ya fedha ya nchi hiyo.
Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tume ya Madini pia umetembelea kitengo cha Gold Jewelry kilicho chini ya Ghana Gold Board, kinachoshughulikia utengenezaji, uthibitishaji, uwekaji alama za thamani na usafirishaji wa bidhaa za usonara.
Kitengo hicho kinatajwa kuwa ni hatua muhimu katika kuongeza thamani ya dhahabu nchini Ghana na kuimarisha ushirikiano wa wadau wote katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.
Ziara hiyo ya kihistoria imeonesha umuhimu wa ushirikiano wa kikanda barani Afrika katika kusimamia rasilimali za madini. Kupitia uzoefu wa GoldBod—bodi pekee yenye mamlaka ya kununua, kuuza, kupima, kuhakiki, kutoa thamani na kusafirisha dhahabu pamoja na madini mengine ya thamani, Tanzania imepata mafunzo muhimu yatakayosaidia kuimarisha mifumo ya usimamizi wa biashara ya madini. Mfano wa Ghana unaonesha kuwa usimamizi thabiti na wa kitaasisi wa sekta ya madini unaweza kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na maendeleo ya taifa kwa ujumla.













Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...