Na Mwandishi wetu
SHIRIKA la INADES-Formation Tanzania limezindua kitalu cha miti chenye lengo la kuzalisha miche 500,000 ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Kitalu hicho, ambacho pia kitazalisha miche ya matunda pamoja na miche ya miti ya asili, kitahudumia Wilaya za Bahi, Kondoa na Chemba, hususan katika vijiji vya mradi wa shirika hilo pamoja na vijiji jirani.
Akizindua mpango huo, Mkurugenzi wa Shirika la INADES-Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus, alisema uanzishwaji wa kitalu hicho utasaidia kuongeza kasi ya kampeni za upandaji miti katika wilaya hizo tatu na kukabiliana na changamoto za muda mrefu za upatikanaji wa miche bora.
Alisema kitalu hicho, ambacho kinaanzishwa kwenye Kituo cha Mafunzo ya Kilimo Mseto katika Maeneo yenye ukame (DATC), kitatumika pia kama kituo cha kuhifadhi miche, kufanya tafiti za miti na kutekeleza shughuli nyingine zinazohusiana na kilimo mseto. Hatua hiyo itaongeza mchango wa shirika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
“Shirika limesukumwa kuanzisha kitalu hiki kutokana na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira, upungufu wa miti na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazozikumba wilaya za Kondoa, Chemba na Bahi,” alisema Nicodemus.
Aliongeza kuwa maeneo hayo ni ya ukame na yamekuwa yakikumbwa na ukataji miti hovyo, uhaba wa miche bora na kupungua kwa rutuba ya ardhi, hivyo uanzishwaji wa kitalu hicho utahakikisha upatikanaji wa miche bora, hususan ya asili, itakayosaidia kurejesha mazingira na kuboresha uzalishaji wa kilimo.
Aidha, alisema upandaji wa miti ya matunda utaongeza kipato cha kaya na kuimarisha ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema shurika hilo limeweka mikakati na miundombinu madhubuti ya uzalishaji wa miche, pamoja na kuwajengea uwezo wakulima, vikundi vya jamii na maafisa ugani kuhusu uzalishaji na utunzaji wa miche ili kuhakikisha lengo la kuzalisha miche 500,000 linafikiwa ifikapo mwaka 2027.
Nicodemus alisema shirika litashirikiana na serikali za vijiji vya mradi, wadau wa mazingira na taasisi za utafiti, pamoja na kutumia teknolojia na mbinu rafiki za kilimo hifadhi, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji na miche katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Ameongeza kuwa mkazo utawekwa zaidi kwenye uzalishaji wa miti ya asili kwa kuwa ina uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira ya ukame, kurejesha mifumo ya ikolojia na kuhifadhi bioanuai. Miti hiyo pia husaidia kulinda vyanzo vya maji na kuboresha rutuba ya ardhi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mafunzo wa Shirika hilo, Bwana Michael Kihwele, alisema upandaji wa miti ya matunda unalenga kuboresha lishe ya kaya na kuongeza kipato huku ukiendelea kuchangia uhifadhi wa mazingira.
Akizungumzia ushirikishwaji wa jamii katika vijiji vya mradi, alisema shirika litatoa mafunzo ya vitendo kuhusu uzalishaji, upandaji na utunzaji wa miche, pamoja na kuunda na kuimarisha vikundi vya mazingira na vitalu vidogo vya miche katika ngazi ya vijiji.
Alisema pia shirika litahamasisha ushiriki wa jamii katika upandaji na ufuatiliaji wa miti iliyopandwa, na kuwawezesha vijana na wanawake kushiriki kama wazalishaji na wasambazaji wa miche.
Hatua hiyo itasaidia jamii kumiliki mradi, kuongeza uelewa wa masuala ya mazingira na kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kitalu hicho kinatarajiwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusaidia kurejesha uoto wa asili, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi maji na kuongeza ustahimilivu wa jamii dhidi ya ukame na majanga ya tabianchi.
Shirika hilo limeendelea kuhimiza wadau kushirikiana na kuunga mkono jitihada hizo kwa kuchukua hatua za vitendo katika kulinda mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
INADES-Formation Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali (NGO) lililoanzishwa mwaka 1989, likiwa ni sehemu ya mtandao wa kimataifa wa INADES-Formation, lenye lengo la kuboresha maisha na ustawi wa jamii za vijijini, hususan wakulima wadogo na wafugaji.
Mkurugenzi wa shirika la INADES-Formation Tanzani, Jacqueline Nicodemus akipokea cheti cha ushindi kwenye maonesho ya Kilimo Misitu wakati wa Kongamano la Kumi la maonesho hayo yaliyofanyika Musoma, Mkoani Mara hivi karibuni

Mkurugenzi wa shirika la INADES-Formation Tanzani, Jacqueline Nicodemus akionyesha cheti cha ushindi wakati wa Kongamano la Kumi wakati wa maonesho ya Kilimomisitu yaliyofanyika Musoma, Mara hivi karibuni.
Mkurugenzi wa shirika la INADES-Formation Tanzania, Jacqueline Nicodemus akishiriki katika kampeni ya upandaji miti wakati wa Kongamano la kumi la Kilimo Misitu lililofanyika Musoma mkoani Mara hivi karibuni. Kongamano hilo lilivutia zaidi ya washiriki 6,000 na kuona miti 860 ikipandwa ambapo wanafunzi wa shule za msingi wilayani humo walishiriki pia




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...