MOSHI.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Shadrack Mhagama, amesisitiza umuhimu wa motisha kwa shule, walimu na wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa kama njia ya kuinua ubora wa elimu na kuhamasisha ushindani chanya.
Mhagama alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa kawaida wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, ambapo shule zilizofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa mwaka 2025 zilitambuliwa na kupongezwa.

Katika hafla hiyo, jumla ya shule sita za Serikali zilitunukiwa vyeti vya pongezi pamoja na zawadi za fedha taslimu kama sehemu ya motisha kwa mafanikio yao.

Kwa upande wa shule za msingi zilizofanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba (PSLE) mwaka 2025, Shule ya Msingi Usagara iliongoza kwa kushika nafasi ya kwanza, ikifuatiwa na Shule ya Msingi Langasani iliyoshika nafasi ya pili, huku Shule ya Msingi Neville ikichukua nafasi ya tatu.

Aidha, kwa shule za sekondari zilizong’ara katika Mtihani wa Kitaifa wa Upimaji wa Kidato cha Pili (FTNA) mwaka 2025, Shule ya Sekondari Kisarika iliibuka kinara, ikifuatiwa na Shule ya Sekondari Kirima katika nafasi ya pili na Shule ya Sekondari Njiapanda iliyoshika nafasi ya tatu.

Mhagama alisema Halmashauri itaendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya kutoa motisha kwa shule vinara kama mkakati wa kuwahamasisha walimu kuongeza bidii katika ufundishaji na wanafunzi kujituma zaidi katika masomo yao.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, John Meela, alisema kuwa Halmashauri itaendelea kutambua na kuthamini mchango wa walimu na shule zinazofanya vizuri, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha maendeleo ya sekta ya elimu ndani ya Wilaya ya Moshi.





 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...