Na WAF, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya Shilingi Bilioni Nne (4) kwa ajili ya matibabu ya upasuaji wa Mabusha nchini ambapo wananchi wanapata huduma hiyo bila malipo.
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema hayo leo Januari 25, 2026 alipofanya ziara kwenye kambi ya upasuaji Mabusha katika Kituo cha Afya Kilakala, Temeke Jijini Dar es Salaam zoezi linaloendelea kwa wiki tatu sasa.
"Serikali imegharamia zaidi ya Shilingi Bilioni Nne katika huduma hii ambapo Upasuaji huu unafanyika kwa kitaalamu, mgonjwa anapewa dawa za usingizi tu sehemu ambayo anafanyiwa upasuaji na ufahamu wake unakuwa upo kama kawaida na," amesema
Aidha, Dkt. Magembe amesema kuwa tangu kuanza kwa kambi za upasuaji wa mabusha katika Mkoa wa Dar es Salaam, zaidi ya watu 1,300 wamejitokeza kupatiwa huduma. Kati yao, watu 668 walithibitika kuwa na mabusha, na watu 457 wamefanyiwa upasuaji, huku lengo likiwa kuwafikia watu 500 katika vituo vya afya vya Kilakala na Kinondoni.
"Ili kujikinga na magonjwa haya ni muhimu kuzingatia usafi wa mazingira ikiwemo kufukia madimbwi ya maji, kufyeka nyasi katika maeneo yanayotuzunguka ili kuzuia mazalia ya Mbu," amesema
Pia, Dkt. Magembe ametumia fursa hiyo kuwaasa wananchi juu ya umuhimu wa Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote kufuatia utekelezaji wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100.
Kwa upande wake Mganga Mkuu Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mohammed Mang'una amewataka wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo kwa kuwa zinatolewa bila malipo ambapo Takwimu zinaonesha kuwa wanaojitokeza zaidi ni wenye umri zaidi ya miaka 45.
Kambi hiyo inafanyika katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo pia itaendelea katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro pamoja na Mbeya.


.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...