
Prof. Habib Mahama ambaye ni Mtaalamu wa Miradi Qatar.
Na Khadija Kalili, Kibaha
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeanza maandalizi ya kuboresha mitaala yake ili iendane na mahitaji ya soko la ajira la kimataifa, hatua inayolenga kuwawezesha wahitimu wake kuajiriwa ndani na nje ya nchi.
Hatua hiyo inakuja kupitia mafunzo ya siku mbili yanayotolewa na Mkuu wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Qatar, Profesa Habib Mahama, raia wa Ghana, kwa wahadhiri wa UDSM. Mafunzo hayo yanafanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Dkt. Theresia Dominic wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amesema Prof. Mahama, ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya miradi, anawafundisha wahadhiri namna ya kuboresha mitaala ili iweze kuendana na viwango vya kimataifa.
“Lengo ni kuhakikisha mabadiliko ya mitaala yanaanza katika ngazi ya chuo kikuu na kushuka hadi ngazi nyingine za elimu, ili wasomi wetu waweze kushindana katika soko la ajira la dunia,” amesema Dkt. Dominic.
Ameongeza kuwa maboresho hayo yatawezesha wahitimu wa UDSM kuajiriwa katika mataifa mbalimbali kutokana na mitaala yao kulingana na ile inayotumika katika vyuo vikuu vingine duniani.
Kwa upande wake, Profesa Omar Mbura, Mkuu wa Shule Kuu ya Biashara ya UDSM, amesema mafunzo hayo yanatoa fursa ya kujifunza kutoka Chuo Kikuu cha Biashara cha Qatar, ambacho kinatajwa kuwa miongoni mwa vyuo 250 bora duniani.
Amesema mbinu zitakazopatikana zitasaidia chuo kuandaa mitaala inayokwenda na wakati, pamoja na kuweka mipango ya muda mrefu itakayoongeza tija na ubora wa wahitimu wa Kitanzania.
“Mabadiliko haya ya mitaala yataifanya UDSM kuwa miongoni mwa vyuo vikuu bora duniani,” amesema Prof. Mbura.
Naye Mratibu wa Mradi huo, Dkt. Mesia Olomo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka UDSM katika Idara ya Elimu na Fedha, amesema mradi huo unalenga kujenga uwezo wa Shule Kuu za Biashara barani Afrika.
Ameeleza kuwa mradi unajikita katika masuala ya utaalamu, masoko, mipango mikakati na namna vyuo vinavyoweza kuzalisha wahitimu bora wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira la kimataifa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...