Yas imeendelea na dhamira yake ya kuwekeza kwenye sekta ya elimu na kukuza vipaji vya vijana wa Kitanzania kupitia udhamini wa wanafunzi kumi mahiri waliochaguliwa kushiriki Kambi Maalum ya Mafunzo ya Hisabati Kigali, Rwanda kuanzia Januari 6 hadi 22, 2026.

Kambi hiyo ya kitaaluma, inayoandaliwa na African Olympiad Academy (AOA) kwa ushirikiano na MIT–Africa, inalenga kuwaandaa wanafunzi wenye vipaji kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kwa ajili ya Mashindano ya Pan-African Mathematics Olympiad (PAMO) yanayotarajiwa kufanyika Juni mwaka huu.

Kupitia taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari, Afisa Mkuu wa Udhibiti Yas, Bi. Sylvia Balwire, alisema udhamini huo ni sehemu ya mkakati mpana wa kampuni katika kuendeleza elimu, ubunifu na teknolojia nchini.

“Kupitia udhamini huu, tunaonyesha msimamo wetu wa muda mrefu wa kukuza elimu na kutengeneza kizazi kijacho cha watafiti, wavumbuzi na viongozi wa teknolojia. Somo la Hisabati ndiyo injini ya uchumi wa kidijitali, ubunifu na utatuzi wa changamoto za kisasa. Kwa kuwaunga mkono wanafunzi hawa, tunawekeza moja kwa moja kwenye mustakabali wa taifa letu,” alisema Bi. Balwire.

Aliwapongeza wanafunzi wote waliochaguliwa, akibainisha kuwa uteuzi wao unaakisi uwezo, nidhamu na kujituma kwa kiwango cha juu katika somo la hisabati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa AOA, Arun Shanmuganathan, alieleza kufurahishwa kwake na ushiriki wa wanafunzi kutoka Tanzania ambao wamepata nafasi ya kuungana na wenzao mahiri kutoka Rwanda, Uganda, Kenya, Botswana, Namibia, Afrika Kusini na Nigeria ambao tayari wanasoma katika taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MIT–Africa, Ari Jacobovits, alisema uwezo mkubwa ulioonekana kwa wanafunzi hao ndio sababu ya MIT kuwekeza kwa kina katika maendeleo yao, popote pale safari yao ya baadaye itakapowapeleka.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Chama cha Hisabati Tanzania (CHAHITA), Dkt. Said Sima, alitoa shukrani kwa Yas kwa mchango wake endelevu katika kukuza vipaji vya vijana na kuinua taaluma ya hisabati nchini.

Wanafunzi hao 10, ambao tayari wamesafiri kuelekea Rwanda kwa maandalizi haya muhimu ya kitaaluma na kimashindano, wanatoka maeneo mbalimbali ya Tanzania na wanawakilisha shule tofauti ikiwemo Ilboru Arusha, St. Francis Mbeya, Feza, Marian, Mahina, St. Monica Arusha na Mbeya Secondary.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...