📍Waibua hoja nyingine ya nyaraka ya kughushi inayoonesha malipo yao


NA MWANDISHI WETU, MUHEZA


BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, limechukua uamuzi mzito wa kihistoria baada ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Dkt. Jumaa Mhina, kwa tuhuma za ufisadi, ubadhirifu wa fedha za miradi kiasi cha shilingi milioni 343 na matumizi ya nyaraka za kughushi.

Uamuzi huo umefikiwa Leo February 27 katika kikao cha Baraza ambapo wajumbe 50 kati ya 51, walipiga kura ya "Hapana" dhidi ya Mkurugenzi huyo, wakidai kuwa ameshindwa kuisimamia Halmashauri na kusababisha hasara kubwa ya mamilioni ya fedha za umma.

Kabla ya Baraza hilo halijakaa leo kupitia Kamati ya fedha, uongozi na Mipango iliitisha kikao januari 20 mwaka huu kujadili mwenendo wa ujenzi wa jengo la utawala na kwamba kikao hicho kilitilia shaka maendeleo ya ujenzi.

Kutokana na kutilia shaka waliagiza mkaguzi wa ndani akakague maendeleo ya jengo na ndiyo ilibobainika kwamba zaidi ya shilingi milioni 343 zimepotea ikiwemo mifuko 700 ya saruji kupotea na vifaa nyingine kununuliwa lakini havikufika 'site'.


Tuhuma za Kughushi Nyaraka za malipo ya madiwani

Moja ya hoja nzito iliyoibuliwa na Diwani wa Kata ya Magila, Mhe. David Kilua, ni madai ya Mkurugenzi kutumia nyaraka za kughushi kuidhinisha malipo hewa. Imeelezwa kuwa Mkurugenzi alitengeneza nyaraka zinazoonyesha madiwani walilipwa posho za vikao vya kugawa jimbo mwaka jana, jambo ambalo madiwani wote walikana mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Tumeitwa TAKUKURU na kuonyeshwa nyaraka iliyoghushiwa ikionyesha tumelipwa posho, wakati ukweli ni kwamba hakuna diwani aliyelipwa hata senti moja. Haya ni malipo hewa yaliyotengenezwa na uongozi," alisema Mhe. Kilua.


Ubadhirifu wa Fedha za Miradi na Jengo la Utawala

Taarifa ya Mkaguzi wa Ndani imefichua madudu mengine, ikiwemo matumizi ya zaidi ya Shilingi Milioni 64 kinyume na maelekezo ya Katibu Tawala wa Mkoa (RAS). Inadaiwa fedha za mradi wa jengo la utawala zilitumika kumlipa mkandarasi anayejenga nyumba ya Mkurugenzi, kinyume na taratibu za kifedha.

Pia, kiasi cha Shilingi Milioni 279 kimebainika kutumika katika matumizi mengineyo, ikiwemo kulipia posho za vikao (Milioni 15) na kazi maalum (Milioni 264), jambo ambalo mkaguzi ameliita kuwa ni matumizi yasiyo sahihi. Aidha, Halmashauri imeingia hasara ya Shilingi Milioni 244 kwa kumuajiri mshauri wa nje wa ujenzi (Consultant) kinyume na kanuni za manunuzi ya mwaka 2024 (Force Account).


Kauli ya Mwenyekiti wa Halmashauri na DC


Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Salimu Shechambo, amesema Baraza limefikia uamuzi huo baada ya kubaini Muheza haipo vizuri chini ya uongozi wa sasa baada ya kupita Waziri Mkuu February 16 mwaka huu.

"Tumetamka rasmi kuwa hatuna imani na Mkurugenzi. Ingawa hatuna mamlaka ya kutengua, tunaomba Mamlaka za Juu zitupe mtu mwingine sahihi wa kufanya naye kazi," alisisitiza Shechambo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza Ayoub Sebabili amekiri kutoridhishwa na hali ya miradi hiyo, akirejea ziara ya Waziri Mkuu ambapo maelekezo ya kusimamishwa kazi kwa watumishi 14 yalitolewa. "Waziri Mkuu alisema tunafumua wilaya yote ianze upya, maana yake hakuna atakayebaki," alisema DC.

Mkurugenzi Aitikia Alhamdulillah

Akipata nafasi ya kuzungumza baada ya "kukataliwa" na Baraza hilo, Dkt. Jumaa Mhina hakuonyesha kupinga maazimio hayo, badala yake alisema: "Sisi tumejifunza kusema Alhamdulillah kwa kila jambo, na kwa kuwa ni mwezi mtukufu wa Ramadhani na Kwaresima, basi niseme Alhamdulillah."

Hatua hiyo sasa inasubiri mwongozo kutoka kwa Waziri wa TAMISEMI na Mamlaka za Uteuzi, huku madiwani wakielekezwa kusimamia miradi katika kata zao ili kuzuia upotevu zaidi wa fedha za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...