Benki ya Exim Tanzania imedhihirisha tena dhamira yake ya muda mrefu katika kuchochea ukuaji na ustawi wa sekta ya utalii kwa kudhamini Z-Summit 2026 kama Mdhamini Mkuu, hafla inayofanyika tarehe 11 hadi 12 Februari 2026 katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA), Tunguu. Hii ni mara ya nne mfululizo kwa Benki ya Exim kudhamini mkutano huu tangu ulipoanzishwa.

Z-Summit imejipatia umaarufu kama jukwaa kuu la biashara na uwekezaji katika utalii Zanzibar, ikiwakutanisha wawekezaji wa utalii, waendeshaji wawatalii, wamiliki wa hoteli, mawakala wa usafiri, watunga sera na watoa huduma kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani. Mkutano huu una mchango mkubwa katika kujenga ushirikiano, kufungua fursa za uwekezaji na kuweka mwelekeo wa maendeleo endelevu ya utalii Zanzibar.

Mbali na akaunti maalum kwa waendeshaji wawatalii na huduma za bima, Benki ya Exim imeendelea kubuni suluhisho za kisasa za malipo ya kidijitali kwa waendeshaji wawatalii. Benki hii ilikuwa ya kwanza nchini Tanzania kuzindua Kadi ya Exim TANAPA, inayowawezesha waendeshaji wa wawatalii kufanya malipo ya kielektroniki kwa ajili ya viingilio vya hifadhi na huduma nyingine. Huduma hii imeboreshwa zaidi na sasa inaruhusu malipo moja kwa moja kutoka kwenye akaunti za waendeshaji wawatalii kupitia mifumo ya mtandaoni kwenda TANAPA na NCAA Safari Portal, hivyo kuongeza ufanisi na kupunguza muda wa miamala.

Zaidi ya hapo, Benki ya Exim imeimarisha mnyororo mpana wa thamani wa utalii kupitia huduma za fedha kwa wasambazaji wa bidhaa na huduma. Huduma hii inawawezesha wasambazaji na watoa huduma katika mfumo wa ikojia ya utalii kupata mikopo ya muda mfupi kupitia mfumo wa kidijitali uliorahisishwa, bila hitaji la dhamana ya ziada. Kwa kuboresha mtiririko wa fedha katika mnyororo wa thamani wa utalii, benki inachangia uendeshaji bora wa biashara na ukuaji endelevu wa sekta.

Ushiriki endelevu wa Benki ya Exim unaonyesha msimamo wake wa kimkakati wa kuunga mkono sekta muhimu kwa uchumi, ajira na upatikanaji wa fedha za kigeni. Utalii ni mhimili wa uchumi wa Zanzibar na benki imeendelea kuwekeza katika suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya biashara zinazojihusisha na utalii.

Kupitia ushiriki wake katika Z-Summit, Benki ya Exim inaendelea kuonesha na kutambulisha suluhisho za kifedha zilizoandaliwa mahsusi kwa ajili ya sekta ya utalii, ikiwemo Akaunti ya waendeshaji wawatalii inayorahisisha miamala ya kielektroniki na usimamizi wa fedha, pamoja na huduma za bima zinazosaidia kupunguza hatari na kuongeza uimara wa biashara za utalii na wawekezaji.

Ikiendana na mkakati wake wa kukuza huduma, Benki ya Exim pia imetangaza mpango wa kufungua tawi lingine Zanzibar ili kusogeza huduma za kibenki karibu na wadau wa utalii, wajasiriamali na jamii. Upanuzi huu unaonesha imani ya benki katika ukuaji wa uchumi wa Zanzibar na dhamira yake ya kuunga mkono biashara na uwekezaji visiwani.

Akizungumza kwa niaba ya benki, Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Shani Kinswaga, alisema kufunguliwa kwa tawi jipya la Paje ni hatua ya kimkakati katika kupanua huduma za benki visiwani Zanzibar na kuimarisha mchango wake kwa sekta ya utalii kama injini ya ukuaji wa uchumi.

“Kwa kusogeza huduma za kifedha karibu na waendeshaji wa utalii, wajasiriamali na jamii zinazozunguka, tunaboresha ujumuishaji wa kifedha na kusaidia ukuaji endelevu wa uchumi unaotegemea utalii Zanzibar. Uwepo wetu visiwani umelenga kutoa huduma za kifedha zinazowawezesha biashara kustawi na jamii kunufaika,” alisema Kinswaga.

Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji wa Utalii Zanzibar (ZATI) Bw. Suleiman Mohammed aliipongeza Benki ya Exim kwa kuendelea kushirikiana na sekta ya utalii, akisisitiza umuhimu wa msaada wa kifedha kwa ustawi wa sekta.

“Msaada wa kifedha ni muhimu kwa uendelevu wa sekta ya utalii. Dhamira ya Benki ya Exim na mipango yake ya kupanua huduma Zanzibar itasaidia kuongeza imani kwa wawekezaji na waendeshaji wa utalii,” alisema mwakilishi wa ZATI.

Kwa kudhamini Z-Summit 2026, Benki ya Exim inaendelea kuonesha nafasi yake kama mshirika wa kimkakati wa sekta ya utalii na mchangiaji mkubwa wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi Zanzibar.








Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...