Bodi ya Maji Bonde la Rufiji kupitia Mradi wa Kuimarisha Mbinu za Asili za Kijamii za Usimamizi wa Vyanzo vya Maji na Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (NBS-USANGU), unaofadhiliwa na Serikali ya Japani kupitia World Bank, imetekeleza mradi wa maji safi katika Shule ya Msingi Jamhuri iliyopo Kijiji cha Ilongo kata ya Ilongo wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.

Mradi huo umezinduliwa na Mwakilishi wa Balozi wa Japan nchini Tanzania ambaye ameonesha kuridhishwa na utekelezaji wake na kusisitiza kuwa ushirikiano kati ya Japani na Tanzania unaendelea kuleta matokeo chanya kwa jamii, hususan katika sekta ya maji na uhifadhi wa mazingira.

Awali, wanafunzi wa Shule ya Msingi Jamhuri walilazimika kutembea zaidi ya kilometa tatu kufuata maji, hali iliyowaweka katika hatari mbalimbali ikiwemo ucheleweshaji wa masomo na uchovu. Kupitia mradi huo, kisima kirefu kimechimbwa na maji kusambazwa shuleni pamoja na kwa wananchi wa maeneo jirani, hatua iliyoboresh­a mazingira ya kujifunzia na kuimarisha usalama wa wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Jenifer Sanga, alisema upatikanaji wa maji ndani ya shule utasaidia kuongeza umakini wa wanafunzi darasani.

“Hii ni faraja kubwa kwetu. Sasa wanafunzi hawatapoteza muda kutafuta maji na wataweza kujikita zaidi katika masomo yao,” amesema Sanga.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilongo, Benjamini Mwakalonge, alisema mradi huo umekuwa suluhisho kwa changamoto ya muda mrefu ya maji katika eneo hilo. “Tunashukuru kwa kuifikia jamii yetu. Maji haya yatasaidia si wanafunzi tu bali pia wananchi wanaozunguka shule hii,” amesema Mwakalonge.

Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, Mhandisi David Munkyala, alisema utekelezaji wa mradi wa NBS USANGU unaakisi dhamira ya bodi hiyo katika kuhakikisha rasilimali za maji zinasimamiwa kwa uendelevu huku zikichochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ameeleza kuwa mradi huo umezingatia pia uhifadhi wa mazingira ili kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Lengo letu si tu kufikisha maji kwa wananchi, bali kuhakikisha tunafanya hivyo kwa njia endelevu inayohifadhi mazingira na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Tunataka miradi hii iwe chachu ya maendeleo ya kweli katika Bonde la Rufiji,” amesema Mhandisi Munkyala.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mradi kutoka Benki ya Dunia, Nicholas Soikan, alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani kuhakikisha miradi ya maji inaleta matokeo yanayokusudiwa.

“Tumeridhishwa na utekelezaji wa mradi huu na tunaamini utaendelea kuleta manufaa makubwa kwa jamii,” amesema Soikan.

Aidha, Mratibu wa Mradi kutoka Bodi ya Maji Bonde la Rufiji, David Muginya, alisema ushirikishwaji wa jamii umekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya mradi huo.

“Tumefanya kazi kwa karibu na viongozi wa kijiji na uongozi wa shule kuhakikisha mradi unakuwa mali ya jamii na unadumu kwa muda mrefu,” amesema Muginya.






Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...