Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mhe. Benjamin Sitta amewapongeza walimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwa kazi kubwa na nzuri ya kuwaelimisha wanafunzi.
Mhe. Sitta ametoa pongezi hizo wakati wa kikao cha tathmini ya elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwenye ukumbi wa shule ya sekondari Tosamaganga.
Katika uboreshaji wa taaluma ya elimu msingi na sekondari Mhe. Sitta amehimiza juu ya umuhimu wa kushirikiana na kuwa na mahusiano mazuri kati ya mkuu wa shule na walimu, walimu na wanafunzi kisha uongozi wa shule na jamii.
Aidha kwenye suala la uboreshaji wa miundombinu ambalo lina sehemu kubwa ya kuinua taaluma Mhe. Sitta amelirudisha kwa Waheshimiwa madiwani ili wakalifanyie kazi kuona kipi ni kipaombele kwenye mahitaji waliyo nayo, hali kadhalika wakuu wa Idara kuwatembelea walimu kwenye maeneo yao ili kujua changamoto zao na kuzitatua.
“Lakini tumekubaliana pia wakuu wa Idara kuwatembelea walimu, wakae nao wawasikilize kwenye changamoto zao, kuna wengine wana changamoto ndogo ndogo ambazo zinaweza kutatuliwa” amesema Mhe. Sitta.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mhe. Steven Mhapa amekiri kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa elimu kwa lengo la kuboresha taaluma na kuahidi Kwenda kuyafanyia kazi kupitia bajeti ya Halmashauri inayoendelea kujadiliwa.
Kwa Upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ndg. Robert Masunya amewakumbusha wadau kuwa yale makubaliano ya wazazi na wananchi juu ya masuala mbalimbali ya kielimu ni sheria tosha kwa ajili ya utekelezaji ilimradi tu zile taratibu zinazohitajika zinafuatwa ikiwa ni Pamoja na mihutasari ya vikao na mikutano na vibali kutoka mamlaka za serikali na kwamba utekelezaji wa makubaliano hayo usiathiri majukumu ya msingi ya mwanafunzi.
Kikao cha tathmini ya elimu Wilaya kimefanyika kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa elimu kujadili suala la taaluma na kutoa motisha mbalimbali kwa waliofanya vizuri na wale waliofanya vibaya.


















Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...