Na Rashid Mtagaluka, Dar es Salaam
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali kwa hatua kubwa inayochukuliwa katika kuimarisha miundombinu ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) nchini, ikisema juhudi hizo zinafungua ukurasa mpya katika matumizi ya nishati safi na nafuu kwa Watanzania.
Pongezi hizo zimetolewa leo jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kamati hiyo katika kituo cha CNG kilichopo Mlimani, ambapo wajumbe walipata fursa ya kujionea maendeleo ya uwekezaji na utoaji wa huduma hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgalu, amesema Serikali imeonesha dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa matumizi ya gesi asilia kwa lengo la kupunguza gharama za nishati na kulinda mazingira.
“Tunapongeza jitihada hizi. Kasi ya ujenzi wa vituo vya CNG inaonesha mwelekeo sahihi wa nchi katika kuhamia kwenye nishati safi. Hata hivyo, tunasisitiza ushiriki mpana wa sekta binafsi ili kuongeza upatikanaji wa huduma hii,” amesema Mgalu.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Wycliffe Makamba, amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati itaendelea kuimarisha miundombinu ya gesi asilia ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma hiyo kwa urahisi.
Amesema matumizi ya CNG yana mchango mkubwa katika kupunguza gharama za uendeshaji wa vyombo vya usafiri na kuchochea ukuaji wa uchumi, huku yakisaidia kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli na dizeli.
Ziara hiyo ni sehemu ya jukumu la kamati hiyo la kusimamia utekelezaji wa sera na mipango ya sekta ya nishati, huku wabunge wakisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza katika nishati mbadala na safi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...