NA FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imetakiwa kuendeleza tafiti bunifu na kuimarisha ujuzi wa watafiti wake, ili kuongeza thamani ya rasilimali za misitu na mazao ya nyuki, na kuhakikisha sekta hizi zinachangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Hamad Hassan Chande mkoani Morogoro wakati wanavunja Bodi ya wakurugenzi TAFORI ambayo imeisha muda wake.
Akizungumza katika kikaohicho Mhe. Chande ameipongeza TAFORI kwa mafanikio makubwa ya utafiti, ikiwemo kubaini sifa za kipekee za asali ya Tanzania, mafanikio hayo yamewezesha pia utengenezaji wa alama ya kimataifa ya Honey Trademark, ikithibitisha ubora wa bidhaa za nyuki zinazotoka nchini.
Aidha ameitaka TAFORI kuendeleza tafiti bunifu, kuongeza thamani ya rasilimali za misitu na mazao ya nyuki, na kushirikiana na wataalamu wa kitaifa na kimataifa ili kuongeza ubora na ushindani wa tafiti zake huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ujuzi wa watafiti kupitia mafunzo ya juu na fursa za uzoefu ndani na nje ya nchi, ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dkt. Revocatus Mushumbusi, ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Bodi ya Wakurugenzi iliyomaliza muda wake, chini ya uongozi wa Mwenyekiti Prof. Verdiana Masanja, kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha taasisi hiyo tangu kuanzishwa kwake.
Dkt. Mushumbusi ameahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri, kwa lengo la kuhakikisha tafiti za TAFORI zinachochea maendeleo endelevu ya rasilimali za misitu na kukuza sekta ya nyuki nchini, huku zikichangia moja kwa moja katika uchumi wa taifa.


.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...