Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma 

Katika shamra shamra za kuelekea Maadhimisho ya miaka 49 ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)wametoa mahitaji mbalimbali kama vile vitanda,sabuni,kanga na kitanda maalum cha joto kwa watoto njiti na wanawake wanaojifungua katika hospital ya Mkoa wa Dodoma.

Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Suzan Kunambi amesema kuwa wao kama UWT ni jumuiya ya wanawake hivyo wana wajibu wa moja kwa moja kuwagusa wanawake na watoto wa Nchi hii kwa kuwasaidia wao na watoto njiti kwani huwezi kumtaja mwanamke ukamuacha mtoto.

Kunambi  ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Februari 3,2026 wakati akimwakilisha Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo  Mary Chatanda katika zoezi la kugawa mahitaji hayo yaliyokwenda sambamba na upandaji wa miti 105 katika eneo la Hospitali hiyo na katika eneo la Shule Msingi Nguji iliyopo kata ya Ng'hong'ona.

"Kama tunavyojua kuwa Jumuiya yetu ni ya wanawake na kazi zetu nyingi zinalenga wanawake,kwahiyo huwezi kumzungumzia mwanamke usimzungumzie mtoto hivyo tukaona mbali ya kupanda miti tukachagua eneo la kuwahudumia wanawake waja wazito na watoto njiti kwa kuwapatia mahitaji japo angalau kutokana na uhitaji uliopo kwa sisi tunao wajibu wa moja kwa moja kuwagusa wanawake na watoto katika nchi yetu".

Aidha Katibu Mkuu huyo amesema kuwa maadhimisho haya si ya kusherehekea tu bali ya kutafakari wajibu wa mwanamke ambao ni nguzo ya familia na Taifa kwani mwananmke anayo nafasi ya kuimarisha maadili ,kulea kizazi chenye uzalendo na kulinda amani ya Nchi.

"Hata hivyo maadhimisho haya si ya kusherekea pekee bali ni ya kutafakari wajibu wetu kama wanawake ambao ni nguzo ya familia na Taifa,tunayo nafasi kubwa ya kuimarisha maadili,kulea kizazi chenye  uzalendo na kulinda amani ya nchi yetu,tunapaswa kusimama imara kupinga vitendo vua ukatili wa kijinsia,ubaguzi na unyanyasaji na kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike na wa kiume".

Pamoja na hayo Suzan Kunambi ameiasa jamii kutokukubali kuchochewa kutumia tofauti za itikadi za kisiasa,kidini na kikabila kwani Taifa hili linalo misingi iliyoasisiwa na waasisi wake ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

Kwa upande wake Mbunge Viti Maalum na Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Dodoma Neema Majule amesema kuwa maadhimisho haya ya Chama kwa Wilaya zote za Dodoma yamekuwa yakifanyika mara nyingi katika Wilaya tofauti tofauti ili kukutana kwa pamoja na kuangazia mambo mbalimbali kwa maslahi ya Taifa. 

Naye John Nchenya akitoa neno la Shukurani kwa niaba ya Mwenyekiti Bodi ya Hospitali ya Mkoa wa Dodoma mara baada ya kupokea vifaa na mahitaji ya wahitaji hao ameshukuru na kusema kuwa kitendo hicho kinaonesha namna gani Chama cha Mapinduzi kupitia umoja wa wanawake wanavyowathamini wananchi wa chini kabisa kwasababu huduma hii waliyotoa inawagusa Watanzania kuanzia ngazi ya chini.

Maadhimisho haya ya miaka 49 ya kuzaliwa kwa chama cha Mapinduzi yanaongozwa na Kauli Mbiu isemayo "Tumechagua Umoja na Amani kwa Maendeleo ya Taifa Letu" na kwa mwaka huu yatafanyika kimkoa February 5 ambapo kwa mkoa wa Dodoma yatafanyika Wilayani Chemba.









 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...