Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeendelea na kampeni yake ya uhamasishaji kwa umma yenye kauli mbiu “Tiketi yako, Haki yako”, kwa kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga kuhusu haki na wajibu wao wanapotumia usafiri huo.

Kampeni hiyo imefanyika katika Kiwanja cha Ndege cha Mwanza tarehe 2 na 3 Februari, 2026, ambapo maafisa wa TCAA waliwafikia abiria na wadau mbalimbali kwa kuwapatia elimu ya ana kwa ana kupitia vipeperushi, mazungumzo ya moja kwa moja pamoja na majibu ya maswali mbalimbali yanayohusu changamoto wanazokutana nazo wasafiri wa anga.

Kupitia kampeni hiyo, TCAA imewaelimisha watumiaji wa usafiri wa anga kuhusu haki zao ikiwemo haki ya kupata taarifa sahihi juu ya safari zao, haki ya fidia endapo safari itachelewa au kufutwa bila sababu za msingi, pamoja na wajibu wa kufuata taratibu na kanuni za usafiri wa anga. Aidha, elimu ilitolewa kuhusu namna sahihi ya kuwasilisha malalamiko yao kwa TCAA ili yaweze kufanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha kuwa watumiaji wa huduma za usafiri wa anga wanafahamu haki zao na wanajua mahali sahihi pa kuwasilisha malalamiko yao pindi wanapokumbana na changamoto, badala ya kukata tamaa au kutumia njia zisizo rasmi.

Katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia Watanzania wengi zaidi, kampeni hiyo pia ilihusisha vyombo vya habari, ikiwemo mahojiano mubashara kupitia runinga ya Star TV na Redio RFA, ili kuwafikia watumiaji wengi zaidi.

Kampeni hii ni endelevu na itaendelea kutekelezwa katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini kama sehemu ya mkakati wake wa kulinda maslahi ya watumiaji wa usafiri wa anga na kuboresha utoaji wa huduma katika sekta ya anga.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...