Na Mwandishi Wetu
Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kimeanza kukutana na jumuiya za shule na Wanafunzi Jiji la Dodoma kwa lengo la kuhamasisha ufaulu hasa katika masomo ya Sayansi.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho na Mwalimu wa Hesabu Dorothy Manoza amesema kuwa jamii imechukulia kama somo la hesabu limekuwa ni shida katika uelewa na kusahau kuwa somo hilo ni somo kama masomo mengi.
Dorothy ameyasema hayo leo Jijini Dodoma Februari 23,2026 katika Shule ya Sekondari Chinangali ambapo Wataalam kutoka NIT wapo katika ziara ya kutembelea baadhi ya shule za Sekondari ikiwemo Drt Samia,Bunge,Hazina,Bihawana,Chinangali na Wella za Jiji la Dodoma ili kuongea na wanafunzi na jumuiya za shule kuhamasisha kuongeza ufaulu katika masomo yao hasa masomo ya Sayansi na kjiunga na fani za masomo hayo wanapojiunga na masomo ya Elimu ya juu.
Ameongeza kuwa wakati mwingine watoto kuogopa Hesabu ni kutokana na kukosa msingi mzuri wa somo hilo,lakini pia wazazi kutowatia moyo watoto hasa mabinti kwasababu tofauti tofauti bila kujua kwamba dunia ya sasa ni ya Sayansi na Teknolojia na hakuna Teknolojia pasipo Hisabati.
"Kweli jamii imekuwa na changamoto ya kuliona kama somo la hesabu ni shida katika uelewa lakini ni kitu ambacho sio sahihi hesabu ni somo kama masomo mengine na unaweza ukafanikiwa kama unavyofanikiwa katika masomo mengine".
Naye Afisa Uhusiano Chuo cha Taifa cha Usafirishaji Juma Mandai ameeleza kuwa wamekuja kuhamasisha umuhimu wa masomo ya Sayansi kwasababu chuo hicho kinatoa kozi inayoenda na miradi mikubwa na ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali na kuhitaji rasilimali watu na Wataalam hususan wazawa ambapo katika miradi hiyo kumekuwa na upungufu wa Wataalamu hasa wazawa wanaoweza kusimamia miradi hiyo.
Na kusema kuwa hicho ndicho kilichowapelekea kuona umuhimu wa wao kama chuo chenye dhamana ya kuzalisha rasilimali watu katika sekta ya Usafirishaji na Uchukuzi kupita katika shule za Sekondari kuhamasisha wanafunzi wapende masomo ya Sayansi na wajue fursa zilizopo katika masomo hayo na kozi zitakazo wasaidia kupata ajira katika sekta hiyo ya Usafirishaji na Uchukuzi.
"Chuo chetu ni cha kisekta kiko chini ya Wizara ya Uchukuzi,tunatoa kozi ambayo inaendana na miradi mikubwa ambayo Serikali inatekeleza kwasasa,miradi ya kimkakati na miradi hii inahitaji nguvu ya rasilimali watu na wataalam ambapo hao wataalam sasa hususan ni wazawa ambapo katika baadhi ya miradi kuna upungufu wa wataalam wazawa ambao wanaweza kusimamia hii miradi ya kimkakati ya Serikali yetu inayotekeleza sasa".
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Chinangali Victor Salisali mbali na kuwashukuru NIT kama wadau wao wa muda mrefu ambao wamekuwa wakiwapatia walimu wa somo la hesabu amesema kuwa ukiangalia masomo ya sayansi yamekuwa na walimu na wanafunzi wachache ila kwa ujio wa NIT utakwenda kuongeza hamasa ya kuwa wanafunzi wengi katika masomo ya Sayansi.
Pamoja na kutoa wito kwa wanafunzi wote kutambua kuwa dunia ipo katika Teknolojia kutoka analogy kwenda digitali hivyo wanatakiwa kuhamasika kufanya au kusoma masomo ya sayansi zaidi ili kuendana na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia.
"Kwa kawaida ukiangalia Walimu wa masomo ya sayansi ni wachache na wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi ni wachache pia, kwahiyo kwa kufika kwenu NIT na kuongea nao nafikiri itakuwa ni hamasa kwao lakini pia tunategemea tutakuwa na wanafunzi wengi ambao watasoma masomo ya Sayansi".
Salim Hassan ambaye ni Kaka Mkuu wa Sekondari hiyo amesema kuwa ujio wa ugeni wa NIT umekuja kuongeza chachu katika masomo ya Sayansi kwa kuwasaidia wale wanaodhani kuwa masomo ya Art tu ndo mapesi hivyo watapendelea masomo ya Sayansi kwani ndio yenye fursa ya ajira.
Naye Sakina Mustapha ambye ni Dada Mkuu katika Shule hiyo pia amesema kuwa hamasa hiyo ya leo inaweza kuhamasisha wanafunzi wengi wakachukua mchepuo wa Sayansi kwasababu NIT imeelezea jinsi mchepuo wa Sayansi ulivyorahisi na utakavyoweza kuja kufanikiwa kuwa Injinia,Rubani na hata kuwa Muhudumu wa Usafiri wa Anga.
Wataalam wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) watakuwa na ziara ya siku 5 kuanzia leo tarehe 23 hadi tarehe 27 februari 2026 na kutembelea Shule 11 za Sekondari kwa Jiji la Dodoma.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...