Na mwandishi wetu, Tanga.
Watumishi wa Wizara ya Nishati wameipongeza Serikali na Wanahisa wengine wa EACOP kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi mkubwa wa kimkakati wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP). Pamoja na pongezi hizo Kampuni ya EACOP imepongezwa kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira katika hatua zote za utekelezaji wa mradi hususani viumbe hai katika maeneo yote yanayopitiwa.
Kauli hiyo imetolewa Februari 22, 2026, Chongoleani, Tanga na mwakilishi wa watumishi hao Bw. Benson Lukuta akiwa Mkuu wa Msafara katika ziara iliyofanywa na watumishi wa Wizara ya Nishati kutembelea mradi huo.
Bw. Lukuta pia kwa niaba ya watumishi aliushukuru Uongozi wa Wizara kwa kufanikisha ziara hii muhimu kwa watumishi kufahamu na kujione Miradi inayosimamiwa na Wizara.
Ziara hiyo ililenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo mkubwa, hususan jinsi unavyozingatia uhifadhi wa mazingira, ulinzi wa viumbe hai katika maeneo yanayopitiwa na manufaa kwa jamii katika maisha ya kila siku na ujuzi.
“Utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati umezingatia sana uhifadhi wa mazingira na kuleta manufaa kwa jamii zinazouzunguka. Mradi huu unaounganisha Tanzania na Uganda na ni mojawapo ya miradi mikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki, ukiwa na lengo la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Bandari ya Tanga, Tanzania,” alisema Lukuta.
Kwa upande wake, Bw. Thomas De Mauleon Mwakilishi wa Kampuni ya EACOP, alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa Watanzania, si tu kiuchumi bali pia kijamii na kitaalamu.
Aidha, amesema mpaka sasa mradi umeweza kutoa ajira za moja kwa moja kwa Watanzania 10,000, huku wananchi 170 wakipatiwa mafunzo maalum ili kufikia viwango vya kimataifa katika ujenzi wa miradi ya mafuta na gesi.
Pia, kupitia miradi ya kijamii, EACOP imeboresha barabara na huduma za maji katika maeneo yanayopakana na Mradi. Takribani kilomita 27 za barabara za changarawe zimeboreshwa, zikiwemo: Barabara ya Kagongwa hadi Sojo (km 18), Handeni kuelekea Kambi Na. 15 (km 2.1), barabara ya kuunganisha eneo kuu la Mradi Chongoleani (km 7.2).
Hatua hizi zinaongeza urahisi wa usafirishaji, kuunganisha jamii na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo yanayopitiwa na mradi.


.jpeg)


.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...