Mwenyekiti wa CEOrt–Roundtable of Tanzania, David Tarimo (kushoto), akimkaribisha Waziri wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, kushiriki maadhimisho ya miaka 25 ya CEOrt yaliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, ameipongeza CEO Roundtable of Tanzania (CEOrt) kwa mchango wake mkubwa katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi nchini kupitia ushiriki wa sekta binafsi, huku taasisi hiyo ikiadhimisha miaka 25 ya kuanzishwa kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Akizungumza wakati wa kufungua rasmi sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya CEOrt, zilizofanyika katika Hoteli ya Hyatt Kilimanjaro, Profesa Mkumbo alisema Serikali inajivunia kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
“Tuna makadirio mbalimbali chini ya Dira ya 2050, na kuna kazi kubwa ya kufanya, ikiwemo uwekezaji mkubwa katika rasilimali watu, ambapo asilimia kubwa ni vijana na hili linaweza kufanikishwa kupitia ushirikiano imara kati ya Serikali na sekta binafsi,” alisema.
Waziri huyo alisema kuwa katika kipindi cha miaka 25 ya uwepo wake, CEOrt imekuwa na mchango muhimu katika kuchochea uchumi wa Tanzania, akisisitiza kuwa ushirikiano endelevu kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu ili kuendeleza kasi hiyo.
Amesema kuwa wakati CEOrt ilipoanzishwa mwaka 2000, Tanzania ilikuwa katika hatua muhimu ya mabadiliko ya kiuchumi, baada ya kuhitimu kutoka kwenye hadhi ya Nchi Maskini Zenye Madeni Makubwa (HIPC) kufuatia mageuzi yaliyoongozwa na Hayati Rais Benjamin Mkapa.
“Wakati huo, tulikuwa bado tunaanza kuingiza dhana ya uchumi wa soko, tukifafanua majukumu ya Serikali na sekta binafsi na pia tulikuwa miaka mitano tu tangu kuanza kwa sera za ubinafsishaji wa uchumi,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri, wakati huo kiwango cha ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) kilikuwa takribani asilimia 4.5, huku Pato la Taifa kwa kila mtu likiwa karibu Dola za Kimarekani 453, na GDP ya jumla ikiwa Dola bilioni 12.37 pekee.
“Ukilinganisha takwimu hizo na tulipofikia leo, tofauti ni kubwa kutokana na mafanikio tuliyoyapata,” alisema.
Alieleza kuwa katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita, uchumi wa Tanzania umeongezeka kutoka Dola bilioni 12.37 hadi takribani Dola bilioni 90, huku GDP kwa kila mtu ikiongezeka kutoka Dola 453 hadi karibu Dola 1,272.
“Ukuaji huu umetokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ukuaji wa biashara, ongezeko la uwekezaji, pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watu,” aliongeza.
Akizungumzia mustakabali wa uchumi, Profesa Mkumbo alisema Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa thamani ya Dola trilioni 1 ifikapo mwaka 2050, lengo litakalowezekana kupitia ushirikiano thabiti kati ya Serikali, sekta ya umma na sekta binafsi.
Alifafanua kuwa makadirio ya awali ya Serikali yalilenga uchumi wa kati ya Dola bilioni 500 hadi 700, lakini baada ya majadiliano, sekta binafsi ilipendekeza lengo kuwa dola trilioni moja.
“Sekta binafsi ilieleza kuwa kwa uwekezaji mkubwa na endelevu, Tanzania inaweza kufikia uchumi wa Dola trilioni 1. Baada ya majadiliano, tulikubaliana na lengo hilo,” alisema.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Bi. Santina Benson, alisema kuwa kati ya mwaka 2005 na 2010, CEOrt iliimarisha ushiriki wake kwa kuwekeza katika uongozi na uimarishaji wa taasisi, hali iliyopelekea kuanzishwa kwa mipango mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Masomo wa Wakurugenzi Wakuu (CEO Scholarship Fund), Mpango wa Kuimarisha Uongozi katika Utumishi wa Umma (EPSL), na Kikosi Kazi cha 3PF, ambacho kilisaidia juhudi za mageuzi katika sekta ya umma, ikiwemo ushirikiano na Mpango wa Mageuzi ya Jeshi la Polisi, pamoja na kutoa elimu juu ya uongozi wa maadili na mapambano dhidi ya rushwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CEOrt, Bw. David Tarimo, alisema kuwa CEOrt ilianzishwa mwaka 2000 katika kipindi muhimu cha mabadiliko ya kiuchumi nchini, wakati kulipohitajika jukwaa la kuaminika la kuwaunganisha viongozi wakuu wa biashara na watunga sera wa Serikali.
“Moja ya mafanikio ya awali ya CEOrt ilikuwa ni mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyoanzishwa chini ya uongozi wa Benjamin William Mkapa, ambayo yaliweka msingi kwamba mafanikio ya maendeleo hupatikana zaidi pale Serikali na sekta binafsi zinaposhirikiana kupitia majadiliano ya wazi, yenye muundo na yaliyojengwa juu ya imani,” alisema.
Katika maadhimisho hayo pia kulizinduliwa Kijitabu cha Urithi wa CEOrt (CEOrt Legacy Booklet), ambapo taasisi hiyo iliwatunuku wanachama wake pamoja na taasisi mbalimbali kwa mchango wao katika safari ya mafanikio ya miaka 25 ya CEOrt.
Miongoni mwa waliotunukiwa Tuzo za Viongozi Wenye Maono (Visionary Leader Awards) ni marehemu Ali Mufuruki, Leonard Mususa, na Yogesh Maneck. Taasisi zilizotunukiwa Tuzo za Mabingwa (Champions Awards) ni pamoja na Vodacom, Stanbic Bank, na Yas Tanzania.
Matukio katika picha katika Mkutano wa CEOrt-Roundtable.
Baadhi ya viongozi na wanachama wa Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEOrt-Roundtable) na wanachama wakiwa uzinduzi wa shehere za miaka 25 ya Jukwaa hilo katika hoteli ya Hyatt Kilimanjaro.



.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...