Mheshimiwa Dkt. Steven L. Kiruswa, Naibu Waziri wa Madini, akipokea kitabu cha kumbukumbu (legacy book) kilichoandaliwa kuadhimisha miaka 25 ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kutoka kwa Lizelle Marwick, Afisa Mkuu wa Sheria wa AngloGold Ashanti na Mwenyekiti wa Bodi ya GGML, wakati wa hafla ya gala ya maadhimisho ya miaka 25, iliyofanyika Hyatt Kilimanjaro, Dar es Salaam.
Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa (kati kati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa mgodi wa dhahabu wa Geita ( Geita Gold Mining Limited-GGML) wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya uwepo wa mgodi huo hapa nchini zilizofanyika Hyatt Kilimanjaro jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa (kulia) akioneshwa picha zilizopo ukutani ( Wall Museum) zilizokuwa zikimuonesha historia ya Mgodi wa Geita Gold Mining Limited (GGML) kutoka kwa Makamu wa Rais wa kampuni mama ya GGML, AngoGold Ashanti, anayehusika na Uendelevu na Mahusiano barani  Afrika, Bw. Simon Shayo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 25 ya mgodi huo hapa nchini iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
SERIKALI imeipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya madini nchini, ikitaja miongoni mwa mambo mengine dhamira yake katika uchimbaji madini unaowajibika, ulipaji kodi, utoaji wa ajira na kushiriki katika maendeleo ya jamii katika kipindi cha miaka 25 ya uendeshaji wake nchini.

Akizungumza katika hafla ya chakula cha jioni ya maadhimisho ya miaka 25 ya GGML iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven L. Kiruswa, amesema rekodi ya utendaji ya GGML inaonesha wazi namna uchimbaji madini unaowajibika unavyoweza kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

“GGML imeonesha kuwa sekta ya madini inaweza kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi pale inapotekelezwa kwa uwajibikaji na kwa ushirikiano kati ya Serikali na jamii,” amesema Dkt. Kiruswa.

Ameongeza kuwa mchango wa GGML kupitia ulipaji kodi, uanzishaji wa ajira na utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) umeimarisha sekta ya madini pamoja na uchumi mpana wa Taifa.

Dkt. Kiruswa amesema uwepo wa GGML unatoa funzo muhimu kwa mustakabali wa ukuaji wa sekta ya madini nchini.

“Kadri Serikali inavyoendelea kutekeleza mageuzi katika sekta ya madini, ushirikiano kama unaooneshwa na GGML ni muhimu katika kuhakikisha maendeleo endelevu na shirikishi,” amesema, akiongeza kuwa GGML imekuwa na mchango muhimu katika kuoanisha sekta ya madini na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.

Hafla hiyo ya hadhi ya juu iliwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali, Wakurugenzi Wakuu wa taasisi mbalimbali, Wakurugenzi Watendaji, wanadiplomasia pamoja na wadau muhimu wa sekta binafsi.

Miongoni mwa waliohudhuria walikuwa viongozi kutoka taasisi za Stanbic Bank, PUMA Energy, Mwananchi Communications Limited, na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Sekta ya madini iliwakilishwa na Chama cha Wachimbaji Madini Tanzania (Tanzania Chamber of Mines) kikiongozwa na Katibu Mtendaji wake, Mhandisi Raymond Rweyemamu, pamoja na wakandarasi wa migodi ikiwemo Suhara Group, wanachama wa jumuiya ya kidiplomasia na wageni mashuhuri wakiwemo aliyewahi kuwa Balozi, Bi. Mwanaidi Maajar.

Maadhimisho hayo yalipambwa na jukwaa la simulizi lijulikanalo kama “Stori za Dhahabu,” lililobuniwa kukusanya na kuhifadhi uzoefu wa watu ambao maisha na shughuli zao zimeguswa na uwepo wa GGML tangu kuanza kwa shughuli zake mwaka 2000.

Jukwaa hilo linaangazia simulizi kutoka kwa wafanyakazi waliodumu kwa muda mrefu, wakandarasi na wanufaika wa miradi ya maendeleo ya jamii inayoungwa mkono na GGML.

Kama sehemu ya maadhimisho, GGML ilizindua filamu ya ‘Stori za Dhahabu’, inayoelezea safari ya mgodi huo kwa kipindi cha miaka 25 na kuonesha simulizi zinazohusu mgodi huo.

Wageni pia walipatiwa kitabu cha kumbukumbu kinachotoa uzoefu wa kipekee unaochanganya simulizi zilizoandikwa na maudhui ya kidijitali.

Akitoa maoni kuhusu mafanikio ya GGML katika kipindi cha miaka hiyo 25, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa GGML na kwa sasa Makamu wa Rais wa Kitengo cha Biashara Afrika katika AngloGold Ashanti, Bw. Terry Strong, amesema GGML ni miongoni mwa migodi inayofanya vizuri zaidi ndani ya kampuni hiyo ( AngloGold Ashanti) barani Afrika.

“Utendaji thabiti wa uzalishaji, nidhamu ya kiutendaji na ushirikiano wa muda mrefu na jamii zinazozunguka mgodi umeifanya GGML kuwa kigezo muhimu ndani ya jalada letu la Afrika,” amesema Bw. Strong.

Hafla hiyo ilihitimishwa kwa tafakari juu ya umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wakandarasi na jamii katika safari hiyo ya GGML kwa kipindi cha miaka 25.

Maadhimisho ya Stori za Dhahabu yameiweka kumbukumbu hiyo ya miaka 25 kama tukio la kukumbukwa linaloonesha umuhimu wa uwekezaji wa GGML katika sekta ya madini nchini Tanzania.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...