Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu, amesema serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeanza mapitio ya kuhakikisha inaweka ada elekezi zitakazotumika kwa vyama vyote vya wafanyakazi nchini ili kuondoa mkanganyiko na kuhakikisha ushindani wa haki katika uendeshaji wa vyama hivyo.

Akifungua kikao cha Baraza la Chama cha Walimu Tanzania (CWT) leo Februari 7, 2026, Jijini Dodoma, Waziri Sangu amesema serikali inalenga kuwa na vyama vinavyowajibika, na vinavyofanya mikutano kwa kuzingatia katiba za vyama pamoja na kuimarisha majadiliano kuanzia ngazi ya vijiji na matawi.

Amesema serikali tayari imeanza mapitio ya mifumo ya uendeshaji wa vyama vya wafanyakazi na itatoa maelekezo ya pamoja yatakayohakikisha vyama vyote vinafuata utaratibu mmoja wa utozaji wa ada badala ya kila chama kujipangia viwango vyake.

Ameongeza kuwa serikali inaheshimu na kuthamini mikataba ya kazi ya kimataifa, huku akisisitiza msimamo wa kuwa na vyama imara na si vyama vya mifukoni, na kwamba hatua kali za kisheria zitaendelea kuchukuliwa dhidi ya waajiri wanaokiuka sheria kwa kuruhusu vyama ambavyo havijakidhi vigezo vya kisheria kuendesha shughuli zao.

Akizungumzia malalamiko ya malimbikizo ya madeni ya walimu, amesema serikali tayari imetoa waraka wa kudhibiti madeni yaliyofanyika kiholela na kuwataka waajiri kuweka mipango ya ulipaji ili kuepusha migogoro baina ya serikali na wafanyakazi.

Kuhusu walimu wanaojiendeleza kielimu kuhesabika kama watoro kazini, Waziri Sangu amesema ofisi yake inalifanyia kazi suala hilo, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na walimu kutatua changamoto zao, huku haki na wajibu vikiendelea kuzingatiwa kwa usawa.

Awali, akisoma risala ya CWT kwa mgeni rasmi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Joseph Misalaba, amesema CWT inaiomba serikali kushughulikia changamoto ya mazingira yasiyo sawa yanayotokana na mkanganyiko wa kisheria, kanuni na miongozo, hali inayosababisha tofauti kubwa za ada kati ya chama kimoja cha wafanyakazi na kingine.

Amesema sheria zinatoa mamlaka kwa chama chenye idadi kubwa ya wanachama kubeba majukumu ya kuwatumikia watumishi katika kada husika, jambo linaloambatana na gharama kubwa za uendeshaji, uajiri wa watumishi na utetezi wa wanachama, tofauti na vyama vingine ambavyo havina wajibu huo na hivyo kutoza ada ndogo zaidi.

Kwa mujibu wa Misalaba, hali hiyo imekuwa ikiwasababisha wafanyakazi kuchagua vyama vyenye makato nafuu bila kuzingatia huduma halisi zinazotolewa, jambo linaloathiri uendeshaji wa vyama vinavyobeba majukumu makubwa kisheria.

Amesema kumekuwa na uwepo wa baadhi ya waajiri wanaoshindwa kusimamia ipasavyo sheria na kanuni kwa kuruhusu vyama kuendesha shughuli bila kukidhi masharti ya kisheria na ya kikatiba, na kuiomba Ofisi ya Waziri wa Kazi kutoa maelekezo ya wazi kwa waajiri wote nchini.

Kwa upande wa Rais wa CWT Suleiman Komba,ameipongeza serikali kwa kuendelea kuajiri walimu wapya katika shule za msingi na sekondari, huku akitoa rai ya kurejeshwa kwa posho ya kufundishia kutokana na walimu kufanya kazi kwa muda unaozidi masaa ya kawaida ya kazi, pamoja na posho za likizo zilipwe kwa wakati kwani Walimu kimsingi ni watulivu, wanaheshimu serikali na kutekeleza wajibu wao.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...