-Rais Samia amhakikishia Rais Museven utayari wa Tanzania katika kushirikiana na Uganda kuleta maendeleo

*Azungumzia ujenzi wa reli ya SGR,atoa ombi kwa Museven,wazungumzia hali ya usalama iliyopo sasa




Na Said Mwishehe,Michuzi Blog.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan ameeleza masuala mbalimbali ambayo wamezungumza na Rais wa Uganda Yoweri Museven huku akimhakikishia utayari wa Tanzania katika kutoa kila aina ya ushirikiano kwa lengo la kufanikisha maendeleo ya nchi hizo mbili.

Aidha amemhakikishia ambavyo Tanzania imejipanga vema katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa kwa lengo la kurahisha usafiri kati ya nchi hiyo na nchi nyingine za Afrika Mashariki ikiwemo nchi ya Uganda.

Akizungumza leo Februari 7,2026 ,Ikulu jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari baada ya kufanyika mazungumzo baina ya marais hao,Rais Dk.Samia amesema katika mazungumzo yao wamejadiliana masuala mbalimbali.

“Tumezungumzia kuhusu bomba la kusafirisha mafuta kutoka Tanzania kupeleka Uganda lakini kuna bomba la mafuta safi sasa ambayo yatakuwa yamesafishwa Uganda yanakwenda kwenye nchi yanayouzwa.

“Tutatumia korido hiyo hiyo kusafirisha mafuta hayo safi kutoka Uganda hadi Tanga na kisha kusafirishwa huko yanakopelekwa.Pili kama mnavyojua nchi zetu ambazo hazina bahari wanategemea sana bandari za Tanzania ikiwemo bandari ya Dar es Salaam na bandari ya Tanga.

“…hata bandari ya Mtwara lakini kwa Uganda ni bandari ya Dar es Salaam na Tanga hivyo tumezungumza jinsi watakavyopata nafasi ya kuzitumia bandari hizi na kusafirisha mizigo.

“Kubwa zaidi tumewapa taarifa Tanzania ndani ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kipindi hiki mpaka 2030 tuna nia ya kujenga reli itakayounganisha Mkoa wa Tanga hadi Musoma na kule watasafirisha kwa ziwa kwenda Uganda.”

Rais Dk.Samia amesema jambo ambalo limewapa faraja sana Uganda wakati wa mazungumzo yao kwani usafiri utakuwa umerahisishwa.

Pia amesema wamezungumza kuhusu reli ya SGR ambayo itajengwa mpaka Isaka na kisha hadi Lusahunga hivyo wamewaomba Uganda waunge hapo kuelekea Murongo na kwenda mbele ndani ya Uganda.

“Hilo ni ombi letu tumewapa ili kuunganisha sasa ile reli iliyokusudiwa kwenda Burundi na DRC sasa tunapeleka mpaka Lusahunga ili Waganda waunge pale kwenda katika nchi yao kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa bidhaa.

“Pia kama mnavyoelewa meli yetu ya MV Mwanza imeanza kufanya kazi ndani ya ziwa na bila shaka itakwenda kuhudumia na Uganda,”amesema Rais Dk.Samia alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akielezea waliyozungumza na Rais Museven .

Pia amesema wamezungumza kuhusu kuondoa vikwazo vya biashara ambapo Amefafanua wamekuwa Wakizungumza mara nyingi kwamba kumekuwa na vikwazo vya biashara ambavyo tumekuwa ukiviondosha.

“Na kila tunapoondosha biashara inakuwa lakini tunakwenda tunarudi nyuma lakini kwa ukweli biashara yetu imekuwa ndani ya nchi zetu za Afrika Mashariki lakini kuna vikwazo ambavyo watendaji wetu katika maeneo mbalimbali wameviweka.

“Tumezungumza kuviondosha ili tukuze zaidi biashara ,tutengeneze soko la Afrika Mashariki na hili ndilo Rais Museven alitumia muda mrefu kulieleza soko la Afrika Mashariki.Wenzetu wa nje wanatuletea vya kwao lakini sisi wenyewe tunazalisha lakini hatuna soko, kwahiyo hilo nalo tumelizungumza kwa kiasi kikubwa.”

Wakati huo huo Rais Samia amesema katika mazungumzo yao wamezungumza kuhusu kuendelea kuzalisha nishati katika miradi ya ushirikiano ambayo inahusisha hayo mabomba lakini utekelezaji wa miradi midogo midogo itakayozalisha nidhati kwa ajili ya matumizi yetu ndani ya nchi zetu

“Lakini kama mnavyojua katika ngazi za kimataifa Tanzania na Uganda tunafanyakazi kwa karibu zaidi na hapa leo tumshukuru sana Rais wa Uganda na timu yake kwasababu mwakani Tanzania ilikuwa na Uganda tunagombania kiti cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Ni zamu yetu kama Afrika Mashariki lakini nilivyomuomba Rais Museven akasema anajitoa, kwahiyo tunawashukuru sana lakini Uganda nayo inagombania kiti kama hicho ndani ya Umoja wa Afrika nasi tumeahidi tunawapa nguvu

“Jingine Rais Museven kwa sasa hivi ni Mwenyekiti wa nchi za Maziwa Makuu na kama mnavyojua ndani ya nchi za maziwa makuu usalama hauko vizuri sana…

“Hivyo anamkakati wa kuanza mazungumzo ya kuleta usalama ndani ya maziwa makuu nasi kama Tanzania tumemwambia tunamuunga mkono na tuko tayari kumsaidia atakavyoona inafaa katika jambo hili,”amesema Rais Dk.Samia

Pamoja na hayo amempongeza Rais Museven kwa kufanya ziara ya kikazi ikiwa ni siku chache baada ya kutangazwa kushinda kwa kishindo nchini Uganda na ziara hiyo imeonesha umuhimu mkubwa wa ajenda za ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda lakini pia kwenye ukanda wetu wa Afrika Mashariki.”

Kwa upande wake Rais wa Uganda Yoweri Museven amemshukuru Rais Samia kwa kumpokea huku akielezea madhumuni ya ukombozi wa Afrika uliokuwa na mambo muhimu matatu likiwemo la kumuondoa Mkoloni ili kuwa huru.

“Baada ya uhuru ikawa kuleta neema kwa wananchi wetu na kwa enzi za sasa neema hizo ni na kuzalisha mali, bidhaa na huduma.“Hivyo unapozalisha mali au bidhaa lazima upate mtu wa kununua. Hivyo kuna haja ya kuwa na soko la uhakika katika Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,”amesema Rais Museven

Pia amezungumzia umuhimu wa kuweka mkakati wa kuimarisha ulinzi na usalama ambapo amesisitiza haja ya kuwa na mkakati madhubuti wa kujihami kwa Afrika .











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...